Na; Amina Pilly
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Muhoja, leo amekutana na watumishi wa sekta ya elimu ya msingi na sekondari pamoja na maafisa watendaji wa kata na mitaa katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Wasichana Songea.
Kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wake wa kawaida wa kukutana na watumishi kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kusikiliza na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao, kujenga mawasiliano ya moja kwa moja, kuimarisha uwazi na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Wakili Muhoja amewataka watumishi hao kuendelea kudumisha nidhamu, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, na kuwajibika ipasavyo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki na stahiki za watumishi ikiwemo likizo, mafao ya likizo, posho, na vitendea kazi.
Alisema kila mtumishi anawajibu wa kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa uadilifu na kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Muhoja huku akihimiza usimamizi madhubuti wa elimu na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa viwango vya kuridhisha.
Kikao hicho kilijumuisha majadiliano ya wazi kati ya uongozi na watumishi, ambapo baadhi ya changamoto na mapendekezo yaliwasilishwa kwa ajili ya kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Songea.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa