Mkurugenzi Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko amewataka wakuu wa shule kusimamia Wazabuni waliopewa kazi ya kupeleka chakula shuleni wahakikishe wanapeleka chakula kilichoongezewa viini lishe ili kuwajengea lishe bora wanafunzi.
Alisema Manispaa ya Songea inaendelea kusimamia na kutekeleza mkakati waliojiwekea wa kuondoa utapiamlo kwa kusimamia Mpango endelevu wa uhamasishaji na uelimishaji kwa jamii ili kujenga mwamko wa kuchangia chakula cha Wanafunzi shuleni pamoja na kuweka katazo kwa Wazabuni kupeleka chakula kisichooongezewa virutubisho.
Dkt. Sagamiko ametamka kauli hiyo akiwa katika kikao cha kamati ya Lishe kilichofanyika tarehe 22 Februari 2023 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wa Lishe kwa lengo la kupitia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Lishe za Halmashauri na kufanya ufuatiliaji wa maazimio yahusuyo shughuli za lishe.
Kwa upande wake Afisa Lishe Manispaa ya Songea Albert Sinkamba alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2022, katika kupambana na udumavu na Utapiamlo, kitengo cha kilifanya uchunguzi wa hali ya Lishe kwa kutumia mzingo wa mkoo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kupima uzito kulingana na umri wa mtoto ambapo jumla ya watoto 49,448 walichunguzwa hali ya lishe kati ya 37,818 sawa na asilimia 153.4%.
Sinkamba alisema kati yao 15 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali sawa na asilimia 0.2 hata hivyo watoto 692 sawa na asilimia 1.3% walichunguzwa na waligundulika kuwa na utapiamlo wa kadiri, pia watoto 48,741 waliochunguzwa sawa na asilimia 98.5% hawakuwa na utapiamlo.
Alibainisha kuwa miongoni mwa mikakati iliyowekwa katika kutekeleza afua za lishe ni pamoja na kuanzisha kituo cha kukusanyia maziwa ya ng’ombe, kuendelea kutoa elimu ya uandaaji wa chakula cha lishe, pamoja na uanzishaji wa klabu za lishe shuleni.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa