WALIMU katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao walipata barua za kupandishwa madaraja na bado hawajarekebishwa mishahara yao wameomba kuvuta subira kwa kuwa serikali kila mwezi inarekebisha mishahara ya walimu waliopandishwa vyeo.
Afisa Utumishi Mkuu wa Manispaa hiyo Lewis Mnyambwa amesema majina ya walimu wote ambao walipandishwa madaraja yao katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 yameingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara na kwamba kila mwezi kuna baadhi ya walimu ambao wanarekebishiwa mishahara yao.
Amesema katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea idadi ya walimu waliopata barua za kupandishwa madaraja ni 704 na kwamba idadi hiyo ni kubwa hivyo walimu wanatakiwa kuwa na subira kwa kuwa serikali imekuwa inarekebisha mishahara yao kila mwezi.
"Sisi kama Idara ya Utumishi Manispaa ya Songea, tumeshakamilisha kazi ya kuyaingiza majina yote kwenye mfumo wa serikali wa utumishi na mishahara,majina ya walimu hao yapo pending kila mwezi kuna walimu wanarekebishiwa mishahara yao,naomba wawe wavumilivu'',anasisitiza Mnyambwa.
Hata hivyo amesema hadi sasa walimu zaidi ya 100 tayari wamerekebishiwa mishahara yao na kwamba suala la kurekebisha mishahara ya walimu waliopandishwa vyeo sasa lipo katika ngazi ya kitaifa hivyo walimu wanatakiwa kuwa wavumilivu.
Akizungumza siku ya sikukuu ya wafanyakazi Mei Mosi mwaka huu iliyofanyika mjini Iringa,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli alisema serikali nchini imewapandisha vyeo wafanyakazi Zaidi ya 88,000 na kwamba wafanyakazi zaidi ya 25,000 wanatarajiwa kupandishwa madaraja yao mwaka mpya wa fedha 2018/2019.
Rais Magufuli aliwahakikishia watumishi kuwa serikali itaendelea kuwapandisha vyeo wafanyakazi kadri bajeti itakavyoruhusu na kwamba watumishi wote wanaodai madeni halali watalipwa fedha zao.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 28,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa