Wananchi Songea kusahau shida ya maji
MRADI wa maji uliofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani Manispaa ya Songea uliogharimu sh.milioni 488.67 unatarajiwa kukabidhiwa kwa wananchi hivi karibuni. Utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwaka wa fedha wa 2013/ 2014 umefikia asilimia 95.Mradi huo unaojengwa na Mkandarasi Giraf Investment Co.Ltd ulitarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hata hivyo mradi huo ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha za kumlipa Mkandarasi kutoka serikali kuu.Mkandarasi wa mradi huo hadi sasa amelipwa sh.milioni 358.36 ambapo katika mwaka wa fedha wa 2016/2017,serikali imeleta fedha kiasi cha zaidi ya sh.milioni 62 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
Kwa upande wake Mhandisi wa Maji katika Manispaa ya Songea Samwel Sanya amezitaja kazi ambazo zimefanyika hadi sasa katika mradi huo kuwa ni ujenzi wa nyumba mbili za mitambo,ujenzi wa bomba kuu la la mm 0.75,bomba la kusambaza maji la mm 9.8,ufungaji wa pampu mbili,ujenzi wa tanki la lita 135,000 na ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji. “Kazi zilizobakia na Mkandarasi anaendelea kukamilisha ni kujenga chemba za pampu na valvu,kujenga vituo vinne vya kuchotea maji,ujenzi wa uvunaji maji ya mvua na kufanya marekebisho yote yaliyojitokeza wakati wa ujenzi’’,amesema Sanya.
Sanya amezitaja changamoto za mradi huo kuwa ni Manispaa kutopata fedha za kukamilisha mradi toka serikali kuu kwa wakati na wananchi kuwa na uelewa mdogo wa uchangiaji na uendeshaji wa miradi ya maji. Watu wapatao 3,447 kutoka katika Mtaa wa Ruhuwiko wanatarajia kunufaika na mradi huo wa maji safi na salama baada ya mradi kukamilika hivi karibuni na kukabidhiwa wananchi kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa