Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kulipa fidia kwa wananchi 878 wa kata ya Mwengemshindo kwa kiasi cha shilingi Bil. 3.7..
Pongezi hizo zimetolewa wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea akiwa katika ziara yake iliyofanyika tarehe tarehe 24 Agosti 2023 Mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la ulipaji wa fidia katika kata ya Mwenge Mshindo Manispaa ya Songea.
Prof. Mkumbo aliendelea kutoa pongezi kwa viongozi wote ngazi ya Mkoa, Wilaya, Diwani wa kata ya Mwengemshindo, vyama vya siasa pamoja na mbunge wa Jimbo la Songea Mjini kwa kufanikisha kulipa fidia kwa wananchi 955 ambao maeneo yao yametengwa kwa ajili ya Uwekezaji EPZA.
Alisema” wabunge huwa wanapimwa kwa sifa nyingi lakini sifa za msingi ni 3 tu ikiwemo na kufahamu mazingira ya wananchi wake, awe anaelewa shida za wananchi wake vizuri, kuwa na Mbunge anayewawakilisha wananchi wake.” Alibainisha.
Alibainisha “ hapo awali mradi wa maji miji 17 Tanzania bara, Songea Mjini haikuwemo lakini kwa jitihada za Dkt. Damas Ndumbaro (MB) mradi huo uliingizwa kwenye bajeti na kuwa miongoni mwa Mji 17 ambapo kwa Songea Mjini mradi wa Maji umetengewa fedha kiasi cha Bil. 145 ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa Songea Mjini.”
Alisema mchakato wa ulipaji fidia ulianza mwaka 2008, Mamlaka ilitwaa eneo lenye ukubwa wa ekari 5000 kwa ajili ya Mradi wa Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Ruvuma (Ruvuma SEZ) katika kata ya Mwengemshindo hadi kufikia mwaka 2023 wananchi hao wamelipwa fidia ambayo ilijumuisha ardhi, mazao, pamoja na nyumba kwa madhumuni ya kujenga viwanda.
Amewataka viongozi kuhakikisha wanatafuta wawekezaji wa kujenga viwanda vikubwa vya kuchakata chokaa kwani chokaa inayotumika kuchakata tindikali inatoka Tanga hivyo hakuna budi kujenga kiwanda hicho katika maeneo ya kata ya Mwengemshindo pia itasaidia kuongeza ajira kwa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi EPZA Charles Itemba alisema Wananchi 966 hawakulipwa fidia katika awamu ya kwanza na kwa mujibu wa uthamini uliofanyika mwaka 2009 jumla ya fidia ilikuwa Tshs. 2,024,319,947.
Kwa mujibu wa sheria kiwango hiki kinapaswa kuhuishwa kwa kuongezwa riba. Riba inayopaswa kuongezwa (compounding interest) kwa kipindi hiki ni 7% kwa mwaka. Hata hivyo, Wananchi 11 kati ya 966 ambao hawakulipwa fidia awamu ya kwanza walilipwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea mwezi Februari, 2023 baada ya halmashauri kuchukua eneo la ukubwa wa ekari 300 ndani ya eneo la Ruvuma SEZ kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ambayo inaeendelea kujengwa, hivyo jumla ya Wananchi 955 ndiyo waliostahili kulipwa katika awamu hii ya pili.
Itemba alisema zoezi la uhakiki lilianza tarehe 3 Agosti, 2023 kwa kuhakiki na usahihi wa taarifa za mali za wananchi kwa kulinganisha na fomu za uthamini, usahihi wa majina ya mfidiwa kwa kulinganisha na yaliyoko kwenye kitambulisho na akaunti ya benki ya mfidiwa hadi kufikia tarehe 16 Agosti, 2023 jumla ya wananchi 878 sawa na 90% walikuwa wamekamilisha uhakiki tayari kwa kulipwa thamani ya Bil. TZS 3,856,676,226.53.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile, ameishukuru Serikali kwa kukamilisha kulipa fidia kwa wananchi wa kata ya Mwengemshindo ambayo ilikuwa ni kero kwa wakazi wa kata hiyo, pia ametoa rai kwa wananchi hao kutumia fedha walizopata kwa maendeleo ya familia yao.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (MB) alitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kulipa fidia ya wananchi wa kata ya Mwengemshindo ambayo ilikuwa kero kubwa wananchi wa Songea.
Dkt. Ndumbaro alisema Serikali imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika mji wa Songea ikiwemo na kuboresha miundombinu ya Maji kupitia mradi wa maji wa miji 17 ambapo wenye thamani ya Bil 145, miundombinu ya elimu, ujenzi wa barabar katikati ya mji KM 10.5, Ujenzi wa Masoko mawili ya Manzese, Mil 600 zilitolewa kulipa fidia uwanja wa ndege Songea, pamoja na Malipo ya fidia kiasi cha Bil. 1.9 katika Bonde la Ruhila Songea. “Alibainisha.”
Kwa upande wa Diwani wa kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea alitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Sulluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha kulipa fidia kwa wananchi wa kata hiyo ambayo ilikuwa kero kwa wananchi.
IMEANDALIWA NA.
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa