Uongozi wa Makumbusho ya Majimaji umewataka wanajamii kutambua umuhimu wa kutembelea Makumbusho ya Mashujaa wa vita vya Majimaji Songea Mkoani Ruvuma.
Mhifadhi kiongozi Adson Ndyanabo ameeleza hayo ofisini kwake katika mahojiano maalumu kuwa Makumbusho hayo yana manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla kwa kuwa yanaongeza mapato na kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wananchi.
Amesema Makumbusho hayo pia yanahifadhi historia,,hutoa elimu kwa jamii ili kutambua tulipotoka, tulipo pia ni utambulisho wa jamii husika .
Ndyanabo amevitaja vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika Makumbusho ya Majimaji kuwa ni Chandamali ambapo kuna mapango yaliyokuwa makazi ya Nduna Songea Mbano, Mahenge ambapo kuna majengo ya Makumbusho, makaburi, sanamu za Mashujaa na vifaa walivyokuwa wakitumia katika maisha yao vikiwemo vya asili na kiutamaduni na Songea Club ambapo Wajerumani walitumia eneo hilo kunyongea Mashujaa.
Amezitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo wito mdogo kwa wanajamii kwani watalii wanaotembelea Makumbusho hayo wengi wao ni wageni , hali ngumu ya maisha imesababisha kupungua kwa idadi ya watalii pia mtazamo wa watu wa elimu bure umeathiri utalii kwasababu imekuwa ngumu kwa wazazi kutoa michango inayowezesha wanafunzi kutembelea vivutio vya utalii kwani wanafunzi walikuwa watalii wakubwa katika vivutio hivyo.
“Kama mtu anashindwa kumtembelea ndugu yake hawezi kutembelea Makumbusho, pia watanzania wengi hawana utamaduni wa kutoka” Amesema Ndyanabo.
Makumbusho ya Majimaji kwa mwaka 2018 na 2019 imetembelewa na wageni wasiozidi 1500 ambayo amesema ni ndogo.Ametoa rai kwa serikali kutangaza vivutio vya utalii kwenye vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi ili kuongeza idadi ya watalii.
Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ni miongoni mwa Makumbusho saba za taifa zilizopo Nchini Tanzania ambayo ilijengwa mwaka 1980.
Imeandaliwa na
Elika Mwakinandi
Wa kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
23 August, 2019.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa