WATU kumi toka katika Kata za Majengo, Misufini, Bombambili,Matarawe na kata ya mjini Manispaa ya Songea wamepigwa faini ya jumla ya shilingi milioni moja na Mahakama ya Mwanzo ya Mfaranyaki baada ya kukataa kulipa shilingi 2000 inayotozwa kila mwezi kwa kila kaya kuchangia usafi wa mazingira.
Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Songea Philipo Beno amesema wameamua kuanza kuchukua hatua ya kuwapeleka mahakamani wananchi wote wanaokaidi kulipa mchango huo hali ambayo inawakatisha tamaa wananchi ambao wanachangia.
‘‘Sheria imepitishwa na wananchi wa Manispaa ya Songea kila mwezi kuchangia shilingi 2000 kwa kila kaya na kwa wafanyabiashara shilingi 4000 ambayo imepitishwa kuchangia usafi wa mazingira katika mitaa na kata za Manispaa’’,anasisitiza Beno.
Amesema wananchi hao kwa nyakati tofauti baada ya kukataa kuchangia kiasi hicho cha fedha walipelekwa mahakamani ambako wamepigwa faini ya shilingi 100,000 kila mmoja kati ya fedha hizo Manispaa inachukua shilingi 50,000 na mahakama shilingi 50,000 na kwamba kuanzia sasa zoezi la kupeleka mahakamani wanaogoma kuchangia usafi wa mazingira litakuwa endelevu.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kupitia kwa maafisa afya kuwapiga faini ya shilingi 50,000 kwa kila mwananchi ambaye hatashiriki usafi Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo ni siku maalum ya kufanya usafi katika maeneo ya umma.
Mgema amekuwa anatoa agizo hilo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kutokana na baadhi ya wananchi kutoshiriki kufanya usafi siku hiyo ambayo imeagizwa kisheria wananchi wote kushiriki.
Sheria ya usafi wa mazingira inawatia hatiani wale wote waliosababisha kuwepo kwa uchafu na wale wanaokataa kufanya usafi wa Mazingira na kwamba adhabu yake ni faini ya sh 50,000 .
Mkuu wa wilaya amewaagiza watendaji wa mitaa kuwaandika majina wananchi wanaoshiriki usafi wa Mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwamba wale wote ambao hawafiki wapigwe faini kulingana na sheria iliyopo.
Mkuu pia amezikumbusha kaya zote katika mitaa 95 ya Manispaa ya Songea kuchangia mchango wa usafi wa Mazingira sh.2000(Elfu mbili) na wafanyabiashara shilingi 4000 ambao unafanyika kila mwezi.
Usafi wa Mazingira ni jambo la lazima ili kukabiliana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu na malaria.
Utafiti umebaini kuwa katika nchi zilizoendelea hakuna watu wanaougua magonjwa yanayotokana na uchafu na kwamba nchi hizo zinashangaa kuona kuna watu wanaugua na kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Machi 26,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa