WATOTO wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 wapatao 28,676 katika mkoa wa Ruvuma wanatarajia kupewa chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi .
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameongoza kikao cha wadau wa Afya mkoani Ruvuma ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ambao wamepitisha azimio la kuanza kutoa chanjo kwa watoto wa kike.
Akizungumza katika kikao hicho Mndeme amewaasa watumishi wa Idara husika kutekeleza zoezi hilo kwa weledi na ameahidi kuchukua hatua za kisheria kwa mtumishi yeyote ambaye atakwamisha zoezi hilo muhimu la kitaifa .
Tanzania mwaka huu imeanza kutoa chanjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana wadogo ili kuwalinda na hatari ya kupata saratani. Ugonjwa wa saratani umeonekana kuwa ni moja ya sababu zinazosababisha vifo hasa kwa wanawake wengi.
Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa kila mwaka watu Zaidi ya 50,000 wanagundulika kuwa na saratani mbalimbali ambako asilimia 30 ya idadi hiyo wanagundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi.
Baadhi ya ripoti zinaonesha kuwa saratani ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo vya akinamama wengi,ikifuatiwa na saratani ya matiti.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo serikali imeanzisha kampeni ya kuwapatia chanjo ya kuzuia saratani ya kizazi kwa wasichana ambapo jumla ya wasichana 600,000 nchini wanatarajia kupata chanjo hiyo.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa