Waziri wa Kilimo Japeth Hasunga amewaagiza watumishi wa wizara yake kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo ili kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Amewataka wataalamu kuzingatia dira ya wizara ili kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara na cha faida kwa wakulima kote nchini.
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo Ijumaa (13.09.2019) wakati alipofanya kikao cha kazi na wafanyakazi wote wa wizara ya kilimo waliopo makao makuu Jijini Dodoma.
“Lengo la wizara yetu ni kuhakikisha nchi inazalisha mazao ya kutosha na kuwa na utoshelevu na usalama wa chakula muda wote” alisema Waziri
Alieleza katika kikao hicho kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umewezesha nchi kuwa na utoshelevu asilimia 124 mwaka 2018 na asilimia 119 mwaka 2019
Waziri Hasunga aliwataka watumishi wa wizara hiyo kuweka mipango inayotekelezeka kitaalam ili kujibu hitaji la wakulima nchini ikiwa ni pamoja na elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija katika eneo dogo.
“Andikeni miradi ili wizara ipate pesa zaidi za kutekeleza shughuli za uzalishaji mazao nchini na badala ya kutegemea bajeti ya serikali ili kufikia tija ya uzalishaji” Waziri Hasunga
Alisema Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali lakini hali ya uzalishaji imeendelea kushuka kila mwaka kutokana na wataalam kutotimiza majukumu yao.
Ili kufikia uzalishaji mkubwa na wenye tija amewashauri wataalam wa wizara ya kilimo kujifunza uzoefu na teknolojia iliofikiwa na nchi za Kenya,Rwanda na Israel ambazo zimepiga hatua kubwa kuzalisha mazao katika eneo dogo.
“Israel, Rwanda na Kenya wanafanya vizuri katika uzalishaji,kajifunzeni ili tubadilishe kilimo chetu kiwe na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa ” alisisitiza Waziri
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza kwenye kikao hicho aliwasihi wafanyakazi kujituma na kutumia vizuri fedha za umma ili miradi inayotekelezwa na wizara iwanufaishe wakulima.
Mgumba aliwataka watumishi hao kuongeza weledi wa ufanyaji kazi ili kupunguza gharama za uzalishaji na mkulima apate bei nzuri ya mazao yake sokoni.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisisitiza suala la matumizi ya Tehama kuzingatiwa katika kuongeza ufanisi wa kazi za wizara ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao na utendaji kazi.
Bashe aliwakumbusha watumishi hao kuwa wizara ya kilimo ndio imeajili watu asilimia 70 hivyo mafanikio ya utekelezaji wa Ilani yakiendelezwa yatasaidia Chama cha Mapinduzi kuendelea kuungwa mkono na wananchi.
“Uwepo wa Chama cha Mapinduzi madarakani utaimarika zaidi endapo sekta hii ya kilimo iliyoajili watanzania wengi itatoa mchango unaokusudiwa katika uchumi”alisema Naibu Waziri Bashe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Matherw Mtigumwe alimshukuru na kumhakikishia Waziri Hasunga kuwa wataalam walio chini yake wataongeza kasi katika ufanyaji kazi ili wizara ifikie malengo ya nchi .
Wizara ya kilimo ina watumishi 974 kati yao watumishi 452 wapo makao makuu na wengine 522 wapo kwenye taasisi, vyuo na wakala nchini.
Imeandaliwa na:
Kitengo wa Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo-DODOMA
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa