WAFANYAKAZI wa Kituo cha Afya Kata ya Mjimwema Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuongeza vifaa na majengo ya wajawazito katika kliniki za watoto ili kukabiliana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika kupata huduma ya afya kwenye kituo hicho.
Muuguzi wa Kitengo cha Wodi ya Wajawazito katika kituo hicho,Ansela Agnery amezitaja changamoto ambazo wanakumbana nazo kuwa ni upungufu wa vitanda hali inayosababisha baadhi ya wagonjwa kulala wawili wawili katika kitanda kimoja.
“Serikali naiomba iongeze jengo na vitanda kwa wajawazito ili kuepusha maambukizi yanayoambukizwa kwa njia ya hewa”.amesema Agnery.
Naye,Mtaalam wa chanjo za watoto katika Kituo hicho,Beatrice Ngwata amezitaja changamoto za vifaa katika kitengo chake kuwa ni pamoja na upungufu wa mabenchi ya kukaa wazazi wanao waleta watoto kupata chanjo.
Licha ya changamoto hizo,Ngwata amesema kitengo chake kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza hali ya kijivu kwa asilimia chini ya 50 na kuongeza hali ya kijani kwa asilimia 80.
Maria Njelekela mgonjwa aliyefika katika kituo hicho cha Afya kupata huduma amewapongeza watumishi hao wa afya kutoa nzuri ambapo ameiomba serika kuboresha kituo hicho kwa kuongeza majengo ili kutoa huduma bora zaidi.
Sophia Maganza Mkazi wa Mjimwema amewapongeza wahudumu wa afya katika kituo hicho kwa kuanza kutoa elimu ya afya kabla ya kutoa chanjo hali ambayo inawajengea uwezo wagonjwa wanaofika kupata huduma ya afya.
Kituo cha Afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8,2002,Kituo hicho kina majengo nane yakiwemo Jengo la wagonjwa wa nje,Wodi ya Watoto na Wanawake,Wodi ya Wazazi na huduma za kujifungua, jengo la kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya Wanaume, jengo la Utawala, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi na jengo la upasuaji.
Imeadaliwa na
Severine Fussi
Wa kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
Agosti 9,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa