WAUMINI wa kanisa la Anglikana Mtaa wa Mtakatifu Augustino Mjimwema Dayosisi ya Ruvuma wamechangia zaidi ya shilingi milioni 113 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa lao.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kanisa hilo kwa Askofu wa Dayosisi ya Ruvuma Mhashamu Raphael Haule,Katibu wa Kanisa hilo Dk.Daniel Mtamakaya amebainisha kuwa kati ya fedha hizo shilingi zaidi ya milioni 111 zimetumika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu zaidi ya milioni 66 zimetumika.
Dk.Mtamakaya amebainisha matumizi ya fedha hizo kuwa zaidi ya milioni 47 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa boma,zaidi ya milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa bati katika awamu ya kwanza na boriti zimetumika zaidi ya milioni 12.
Matumizi mengine kulingana na Katibu huyo wa Kanisa,ni shilingi milioni nne gharama za fundi wa kuezeka,madirisha zaidi ya milioni 10 na kwamba kiasi kingine cha fedha kimetumika kwa ajili ufundi gibro,miundimbinu ya kanisa,umeme,mchanga,nyumba ya padre,kokoto,saruji na nondo.
“Kanisa limefanikiwa kununua ardhi yenye ukubwa wa hekari 100,kanisa limefanikiwa kusimamia kwaya yetu ya Mtakatifu Augustino kurekodi video,tunatarajia uzinduzi wa kwaya hiyo kufanyika hivi karibu,pia kanisa linaendesha semina za ndani kwa viongozi wa kanisa’’,amesisitiza Dk.Mtamakaya.
Kwa upande wake Padre wa Mtaa wa Kanisa hilo Padre John Midelo ameyataja matarajio ya kanisa hilo kuwa ni kuanza maandalizi ya ujenzi wa zahanati na uanddaaji wa mashamba mara baada ya ukamilishaji wa Hati.
Amesema kanisa linafanya ushirikishaji mkubwa kwa waumini katika kuendeleza kanisa na kwamba mkazo umewekwa kila waumini wanaoishi bila ndoa,wanashauriwa kufunga ndoa.
“kanisa hili linategemea zaidi rasilimali watu(waumini) katika kupata mapato yake ambapo mahudhurio katika ibada yamekuwa ni wastani wa waumini 106 ambao wanatoa wastani wa zaidi ya shilingi 80,000 kila siku ya bwana’’,anasisitiza Padre John.
Akizungumza katika Ibada ya utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 26 katika kanisa hilo,Askofu Haule amewapongeza waumini hao kujenga kanisa kubwa na linalovutia na kwamba hilo limewezekana kutokana na kusimama katika imani.
“Kilichowasimamisha hadi kujenga kanisa hili ni imani,kwa hiyo kwa imani tunaweza kufanya mambo makubwa ambayo,ndiyo maana Mungu amemleta roho Mtakatifu ili kukuza imani yetu’’,amesisitiza Askofu Haule.
Imeandaliwa na Albano Midelo,mawasiliano 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa