WAZEE WALIA NA KERO YA MATIBABU
WAZEE katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameitaja kero ya kupata matibabu bure inaongoza kwa wazee hali ambayo inasababisha wazee wengi kukosa matibabu.
Akisoma risala ya wazee siku ya maadhimisho ya siku ya wazee duniani Oktoba mosi mwaka huu,Makamu Mwenyekiti wa Baraza Huru la Wazee wa Manispaa ya Songea Sophia Hasara,ameiomba serikali kuwapatia wazee kadi za matibabu bure kama ilivyoelezwa na serikali.
Amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa kadi za matibabu bure kwa wazee wote wa Manispaa hiyo ili kumaliza kero hiyo ambayo inasababisha baadhi ya wazee kupoteza maisha kwa kushindwa kugharamia matibabu.Hata hivyo wazee hao wameipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo wamesema bajeti hiyo pia itawanufaisha wazee wa Tanzania.
Katika risala yao wazee wamelaani matukio ya mauaji ya wazee,utekaji nyara wa watoto na mashambulio mbalimbali yanayotokea kwa viongozi na kwamba ili kukabiliana na matukio hayo wameshauri serikali kukaa na wazee ili waweze kupata mawazo ya nini cha kufanya kuondoa taharuki hiyo.Wamesema ni wajibu wa serikali ya awamu ya tano kushirikisha wazee wa kada mbalimbali ili waweze kutumia ujuzi,uzoefu na michango ya mawazo kufanikisha malengo mbalimbali ya serikali.
Wamebainisha kuwa ingawa wazee hawana nguvu nyingi,hata hivyo kwa kutumia hekima na busara zao wanaweza kuelekeza,kushauri na kusimamia kwa ufanisi lengo kuu la awamu ya tano la kuwa na serikali ya viwanda ili kuleta maendeleo kwa watanzania.Wazee hao wamesisitiza mshikamano,umoja na juhudi ili kufikia lengo lililowekwa na serikali la hapa kazi tu na kusisitiza serikali itunge sheria ya wazee ili kuwezesha wazee kunufaika na sheria hiyo kwa kuwa sera ya wazee pekee yake haina uwezo wa kutatua changamoto za wazee.
“Sisi wazee wa Manispaa hatujanufaika lolote na sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 kwa sababu sera hiyo haina meno kwa kuwa haijatungiwa sheria’’,inasema risala ya wazee hao.Wamemuomba mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mbunge wa Songea mjini Leonidas Gama kuwafikishia kilio cha kutungwa sheria ya wazee Bungeni Dodoma na kwamba hawaoni sababu za msingi za kucheleweshewa kutungiwa sheria hiyo wakati sera imedumu muda mrefu.
Kulingana na takwimu za wazee za mwaka 2016,Manispaa ya Songea ina zaidi ya wazee 11,000.Maadhimisho ya wazee ya mwaka 2017 ni ya 19 ambapo maadhimisho ya kwanza yalifanyika mwaka 1999,kauli mbiu ya mwaka huu ni Kuelekea Uchumi wa Viwanda,Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee kwa Maendeleo ya Taifa.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo,Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa