WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amewatoa hofu Wakazi 1,000 wa eneo la Mwengemshndo Manispaa ya Songea wanaodai fidia ya Tshs. Bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa kwa ajili ya Ujenzi wa Viwanda.
Waziri Mkuu Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatambua kilio chao ambacho amesema ni cha muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa Mbunge wao wa zamani, Bw. Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu.
...........“Alipotoka kutibiwa India alikuja ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi. La kwanza lilikuwa ni hili la fidia kwa wakazi wa Mwengemshindo, na la pili lilikuwa ni la Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Mjini Songea”..alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga Viwanda Vitatu.
“Kutakuwa na kiwanda cha kusindika Mahindi, kutengeneza Pumba za Kuku na Ng’ombe na Mbolea. Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika Kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha kukamua Mafuta ya Mbegumbegu,” alisema Waziri Mkuu.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa malipo yao, Waziri Mkuu alisema kwamba katia ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni Mwekezaji mmoja tu, na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa ulipaji kwa sababu walifuata orodha ya majina (kialfabeti) badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika.
Ameongeza kuwa Mwekezaji anataka kuanza Ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe.
Ameahidi Serikali kuwafuatilia wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia waweze kulipwa
Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa uthamini Mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 3.25 Kuanzia Juni 2015,ambapo Serikali iliwalipa wakazi 1,179 Kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kati ya hizo,bilioni 1.2 zilikuwa ni Malipo ya thamani ya Mali za wananchi na zaidi ya milioni 710 zilikuwa ni RIBA kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.
Eneo la Mwengemshindo lenye ukubwa wa Hekta 2,033 lilitwaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Ruvuma, na Manispaa ya Songea tangu Mwaka 2007. Eneo hilo linajumuisha Mitaa ya Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na Luhira.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa