Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
14.04.2022
Waziri wa habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari, Nape Moses Nnauye amewataka wananchi kushirikiana na viongozi Mkoani Ruvuma kutumia zoezi la anwani za makazi kuwaenzi waasisi katika maeneo yao ili kulinda historia yao.
Nape aliyasema hayo hapo jana Aprili 13, 2022 katika ziara yake ya kukagua zoezi la anwani za makazi Mkoani Ruvuma ambapo ameelekeza kutumia zoezi hilo kwa kuenzi historia ya nchi kwa kutaja majina ya viongozi na maarufu katika maeneo ya mitaa na barabara kubwa kutokana na utendaji kazi wao katika kutengeneza historia ya nchi.
Alisema “Nimekuja Ruvuma kukagua na kuona zoezi hili linaendeleaje na nina furaha kubwa katika Mikoa inayofanya vizuri, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inyofanya vizuri katika zoezi hili” Nape alibainisha.
Aidha, ametoa wito kwa Wakala wa barabara mijini (TANROADS) na Wakala wa barabara vijijini (TARURA) kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kukamilika kwa wakati ili kusaidia kuweka majina na alama katika barabara zao.”Alisisitiza”
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na linatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 30, 2022 na hivyo umakini utaongezeka katika kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.
Akitoa takwimu za Mkoa wa Ruvuma katika utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi kitaifa Afisa Tehama Mkoa wa Ruvuma Yahaya Madenge alisema kuwa, hadi sasa Mkoa wa Ruvuma umeshika nafasi ya kumi Kitaifa katika utekelezaji wa zoezi hilo kwa kufikia zaidi ya asilimia 96%.
Kwa upande wake Afisa Tehama Manispaa ya Songea, Mvano Mbalale alisema kuwa zoezi hilo kwa Halmashauri ya Mnaispaa ya Songea limefanyika kwa weledi mkubwa ambapo wananchi walitoa ushirikiano kwa wataalamu waliofanya zoezi la ukusanyaji wa taarifa katika maeneo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Mh. Diwani Jeremiah Milembe (Naibu Meya Manispaa ya Songea) alieleza kuwa zoezi hilo ndani ya Manispaa ya Songea litakamilika kabla ya kufikia tarehe husika iliyopangwa na Mkoa na hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa