HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetengeneza Mpango Kabambe (General Planning Scheme) wa miaka 20 (2016-2036) katika maeneo ya uwekezaji na utalii.
Mchumi Mkuu wa Manispaa ya Songea Raphael Kimary anasema kuna hekari 5,000 katika eneo la Mwengemshindo, na eneo la viwanda vya huduma hekari 150 katika kata ya Lilambo ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji.
Kimary anasema Halmashauri imetenga hekari 2.5 katika eneo la Namanditi kata ya Ruhuwiko kwa ajili ya Machinga na kwa sasa hekari mbili zimetengwa na zinatumika na Machinga katika eneo la Majengo Greenbelt.
Anasema Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya misitu ya hifadhi 10, kati ya hiyo misitu 3 (West Matogoro 1000.5ha, East Matogoro 7457.24ha na South Matogoro 6755.7ha) ni ya Serikali Kuu inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na misitu 7 (Likuyu 722ha, Kwalikucha 33ha,Namanyigu 7.1ha,Chandamali 29ha,Liumbu 66.8ha na Unangwa 20ha, Nangwai 72.9ha)
“Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira imepanda jumla ya miti 925,146 katika Misitu ya hifadhi Matogoro, vyanzo vya maji vya bonde la mto Ruhila na milima ya Kwalikucha-Liwena. ilitoa kwa wadau jumla ya kilogramu 112 za mbegu za miti na viriba kilogramu 200’’,anasema Kimary.
Amesema halmashauri ina mizinga 1040 ya ufugaji Nyuki inayo milikiwa na vikundi,taasisi na ya watu binafsi. Hali hii inasaidia kuboresha vyanzo vya maji,kuboresha mazao ya misitu na zao la asali ambapo litasaidia kuongeza kipatocha wananchi.
Kulingana na Mchumi huyo, Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina hifadhi moja ya wanyamapori ambayo ni hifadhi ya Ruhira (Ruhira game reserve) inayosimamiwa na Kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini (KDU) chini ya Mamlaka ya Kusimamia Wanyamapori Tanzania (TAWA)
“Kazi kubwa ya sekta ya wanyama pori ni kulinda na kuhimiza ulinzi wa wanyama pori ambao ni hazina ya nchi yetu. Vilevile ni jukumu la sekta kulinda na kuendeleza hifadhi ya wanyamapori katika pori la akiba Ruhira, Kulinda mali na maisha ya wananchi kutokana na wanyama wakali na waharibifu, na uhamasishaji, uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori katika mitaa inayozunguka pori pamoja na kufanya doria kwa kuzuia ujangili’’,anasema Kimary.
Hata hivyo anasema Halmashauri ina fursa na vivutio vingi vya utali ambavyo husababisha matukio mbalimbali ya shughuli za utalii na za kiutamaduni kufanyika kama vile, Tamasha la Kitaifa la kumbukizi la vita vya majimaji linalofanyika kila mwaka kuanzia 25 Februari mpaka tarehe 27 Februari ambayo ni siku ya kilele na ni siku ambayo walinyongwa mashujaa wa vita vya majimaji.
Analitaja tamasha jingine ambalo linafanyika kila mwaka katika Manispaa ya Songea kuwa ni tamasha la majimaji serebuka pia linaloendeshwa na NGO’s ya Songea Mississippi shughuli zinazofanyika ni maonesho ya ujasiliamali, mashindano ya ngoma za asili, study tour, mbio za marathoni, mbio za baiskeli, fiesta na maonesho ya mashujaa wa vita vya Kagera.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Novemba 6,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa