Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni kati ya Halmashauri 8 za mkoa wa Ruvuma yenye jumla ya wakazi 281,217 ikiwa wanaume 132,171 na wanawake 149,046.
Ikiwasilisha taarifa ya hali ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea hadi mwezi Machi 2021 kwenye kikao cha wajumbe wa kamati ya maji na usafi wa mazingira, watendaji wa kata na maafisa afya wa kata pamoja na wadau mbalimbali wa usafi na mazingira, katika ukumbi wa Manispaa ya Songea tarehe 24 Juni 2021.
Afisa afya wa Manispaa ya Songea Maxensius Mahundi alisema kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira ndani ya Manispaa ya Songea kuanzia mwaka 2012/2013 hadi mwaka 2020/2021 ni pamoja na kufanya mikutano ya uhamasishaji (kuchefua) na ufuatiliaji katika jamii kwa mitaa yote 95, kutoa mafunzo elekezi kwa mafundi uwashi 51 kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya ujenzi wa vyoo bora, kuendesha mashindano ya afya na usafi wa mazingira kwa kata 21 na kukusanya takwimu za hali halisi ya usafi wa mazingira katika kata zote zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kipindi cha kila robo mwaka.
Awali yalitolewa mafunzo kuhusu kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kwa waratibu elimu kata 21 juu ya ukarabati, ujenzi wa vyoo na uwekaji wa miundo mbinu ya kunawa mikono nje ya vyoo katika kipindi cha kila robo mwaka. “Alieleza”
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira ni pamoja na wananchi kutojenga vyoo bora, kutoweka miundo mbinu ya kunawa mikono nje ya choo kwa hiyari bali huhitaji shuruti, kutokuwepo kwa uzio katika shule nyingi za msingi, baadhi ya wakazi huharibu miundombinu ya vyoo vya shule kwa kuiba mabomba ya kutolea hewa chafu kutoka kwenye vyoo, ukosefu wa maji ya kudumu kwa baadhi ya shule za msingi pamoja na ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa watumishi wa ngazi ya kata kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira.”Mahundi Alibainisha”
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Phillipo Beno alisema kwamba Halmashauri imejipanga kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa usafi wa mazingira, kuhamasisha jamii kuweka ulinzi shirikishi na kuweka uzio katika shule, kufanya ukaguzi na kubainisha kaya zisizo na vyoo bora katika mitaa, pamoja na kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria wakazi wa Manispaa ya Songea wasio na vyoo, wenye vyoo vibovu, wasioweka miundombinu ya kunawa mikono nje ya choo.‘Alisisitiza’
Hadi sasa jumla ya kaya 63,913 ambayo ni sawa na asilimia 100% katika Manispaa ya Songea ambazo zimefikiwa na kampeni ya usafi wa mazingira tayari zina vyoo ambapo katika kaya hizo, kaya 57,458 sawa na asilimia 89.9% zenye vyoo bora na kaya 6,455 sawa na asilimia 10.1% ambazo bado hazina vyoo bora.
“USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO”
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
29.06.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa