Siku ya wauguzi Duniani ( International Nurse Day) huadhimishwa ulimwenguni kote kila mwaka tarehe 12 Mei wakikumbuka na kutafakari mchango wao wanaotoa kwa jamii.
Siku hiyo iliibuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1953 na Dorothy Sutherland aliyekuwa Afisa kutoka kitengo cha Elimu ya Afya na Ustawi Nchini U.S kwa lengo la kuangalia mchango wa Wauguzi katika kuhudumu jamii.
Baraza la Wauguzi Ulimwenguni (International Council of Nurse) ilianza kuadhimisha siku hiyo tangu mwaka 1965 na mwaka 1974 Januari ambapo ilitolewa tamko rasmi kuwa Siku ya Wauguzi Duniani iadhimishwa Ulimwenguni kote tarehe 12 Mei.
Hayo yalibainishwa kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kiwilaya katika Viwanja vya Mjimwema Kituo cha Afya na kuhudhuriwa na Wauguzi, pamoja na wadau mbalimbali wa afya.
Akizungumza Afisa Elimu Manispaa ya Songea Mwl. Janeth Moyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea alisema Chama cha Wauguzi Tanzania Tawi la Manispaa ya Songea kinaendelea na jitihada za makusudi za kukemea wauguzi wanaofanya kazi kinyume na makubaliano, kanuni na Sheria za kazi ya uuguzi, wauguzi kwani sio wauguzi wote ambao si waadilifu kwa wagonjwa n a jamii kwa ujumla. Alibainisha.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kazi ya muuguzi pamoja na kuwawezesha wauguzi kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya Taaluma na maadhimisho ya kimataifa ya siku ya Wauguzi pamoja na kuajiri watumishi wa ajira mpya.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu Manispaa ya Songea Theodosia Ngowoko alisema Kauli Mbiu ya mwaka 2023 ni WAUGUZI MUSTAKABALI WA AFYA YETU” OUR NURSES OUR FUTURE” Kauli mbiu hiyo inaangazia umuhimu wa kuwalinda Wauguzi, kuwekeza katika fani ya uuguzi na kuheshimu haki za Wauguzi kwa kujenga mifumo thabiti ya Afya ya hali ya juu ili kukidhi mahitaji ya jamii.
Ngowoko aliongeza kuwa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo shughuli mbalimbali za kijamii bila malipo zilifanyika ikiwemo na upimaji wa VVU, Huduma ya Uzazi wa Mpango, Uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa kizazi, Kutoa huduma ya Tohara, ambapo shughuli hizo zilianza kuadhimishwa kuanzia tarehe 10 Mei 2023 hadi siku ya kilele tarehe 12 Mei 2023. Alibainisha.
KAULI MBIU YA 2023; WAUGUZI MUSTAKABALI WA AFYA YETU” OUR NURSES OUR FUTURE”
Imeandaliwa na;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa