Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
25 JULAI 2022
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (MB) ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuunga mkono Tamasha la Majimaji Serebuka ambalo linasaidia kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni nchini Tanzania.
Akizungumza katika uzinduzi wa Tamasha la Majimaji Serebuka msimu wa nane uliofanyika tarehe 23 Julai 2022 katika uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea, Mhe. Gekul alisema kuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inaendeleza pamoja na kulinda utamaduni nchini.
Aliongeza kuwa kwa mwaka fedha 2022/2023 Wizara imeweka vipaumbele mahususi kwa utekelezaji wa mfumo wa utamaduni na sanaa unaolenga kuwanufaisha wadau wa sekta ya sanaa nchini pamoja na kuanzisha Tamasha la utamaduni la Kitaifa ambalo lilifanyika kwa mara ya kwanza Julai 1, 2022 jijini Dar es salaam.
Mhe. Gekul ametoa wito kwa viongozi wa Mikoa mingine nchini kuanzisha matamasha ya utamaduni katika Mikoa yao ili kuhakikisha yanaenea nchi nzima na kusaidia kukuza sanaa na utamaduni wa Taifa kwa ujumla.
Ametoa rai kwa viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni mbalimbali yatakayosaidia katika zoezi la uandaaji wa kitabu cha muongozo wa maadili ya Taifa la Tanzania ambacho kinalenga kupambana na mmong’onyoko wa maadili nchini kwa kuendeleza utamaduni wa Taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Muanzilishi wa Tamasha la Majimaji Serebuka Mhe. Damas Ndumbaro Waziri wa Katiba na Sheria (MB) alibainisha kuwa “Hili ni Tamasha la nane kufanyika tangu kuanza kwa Tamasha la Majimaji Serebuka ambapo litafanyika kwa muda wa siku nane”.
Ndumbaro ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushuhudia muendelezo wa Tamasha hilo kwa siku zilizobaki ambapo hakuna kiingilio ni bure kabisa.”Alisisitiza”
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Kamando Mgema (Mkuu wa Wilaya Ya Songea) alisema kuwa tamasha la Majimaji Serebuka linasidia kuamsha Ari ya wanaruvuma kutambua, kuthamini na kuendeleza urithi wa utamaduni wa Mtanzania pamoja na kutoa fursa za ukuaji wa uchumi kwa wajasiriamali waliojitokeza kushiriki katika Tamassha hilo.’Alibainisha’
Pololet aliongeza kuwa Tamasha hilo linasidia kutangaza fursa za utalii na uwekezaji ziliopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na kuchochea mchango wa sekta ya Sanaa, utamaduni na Michezo katika maendeleo ya jamii.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa