Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini kikiongozwa na Mwinyi MSolomi ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, tarehe 03 Septemba 2023 umefanyika uzinduzi wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Udiwani kata ya Mfaranyaki kwa lengo la kutangaza Mgombea wao ndugu Christopher Kayombo ambaye anagombea nafasi ya Udiwani katika kata ya Mfaranyaki kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Uchaguzi huo umekuja mara baada ya kutokea kwa kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata ya Mfaranyaki Marehemu Ajira Kalinga ambaye alifariki Dunia tarehe 06 Mei 2023 katika Hosptali ya BOCHI Jijini Dar es salaam na kuzikwa katika Makaburi ya Mfaranyaki Mjini Songea.
Aidha, miongoni mwa vyama vya Siasa vilivyogombea katika nafasi hiyo ni Chama cha Mapinduzi “CCM” UDP, ACT WAZALENDO, Chama cha Wananchi CUF, AAFP, pamoja NCCR MAGEUZI.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komredi Oddo Mwisho alisema CCM imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi yenye ukurasa 303 ambapo kwa Manispaa ya Songea kupitia kata ya Mfaranyaki kuanzia mwaka 2020 imetekeleza miradi mingi ikiwemo na miundo mbinu ya Elimu kupitia ujenzi wa madarasa kwa Shule za Msingi na Sekondari, Sekta ya Afya, Masoko, pamoja na Ujenzi wa Barabara za mitaa katika Kata ya Mfaranyaki ambao unatarajia kuanza hivi karibuni.
Aliongeza kuwa, Chama cha Mapinduzi ni chama pekee chenye kutetea haki za wananchi, ambapo kutokana na ubora wa utendaji kazi imara walipokea wanachama wawili 2 kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambao walirudisha kadi za CHADEMA na kupokea kadi za CCM mbele ya wanachama wa CCM, na wananchi waliohudhuria mkutano huo ambao ulifanyika katika uwanja wa Stendi ya Lori kata ya Mfaranyaki.
Kwa upande wake Mgombea Christopher Fabian Kayombo alitoa shukrani kwa wanachama wa CCM kwa kumpitisha na kumpa ridhaa ya kugombea katika nafasi ya Diwani kata ya Mfaranyaki, na kuahidi kuwatumikia wananchi wa kata hiyo mara atakapochaguliwa kuwa Diwani wa kata ya Mfaranyaki, hatimaye aliomba kura kwa Wananchi.
Hata hivyo, mara baada ya mgombea kuomba kura kwa wananchi, Komredi Oddo Mwisho alimkabidhi Ilani ya CCM kwa ajili ya ufuatiliaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kata ya Mfaranyaki iliyoanzishwa na ambayo haijaanzishwa utekelezaji wake kuanzia kipindi cha Uhai wa aliyekuwa Diwani wa kata hiyo hadi hivi sasa ili aweze kusimamia na kutatua changamoto za kata hiyo.
Uchaguzi mdogo wa Diwani unatarajia kufanyika tarehe 19 Septemba 2023.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa