Kamati ya siasa CCM Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kutembelea kata ya Lilambo na kukagua Mradi wa Maji Lilambo A na Lilambo B, ambao umesanifiwa na kuhudumia Wakazi wapatao 11,981 ambao ulianza kutekelezwa 28/05/2019 na kukamilika 31/03/2020 chini Mkandarasi PNR Services Limited Dar es salaam.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akiwakilishwa na Mjumbe wa Mkutano MKuu CCM Taifa Mussa Homera Katika ziara ya kutembelea Miradi iliyofanyika 08/07/2020 Manispaa ya Songea, ambapo alianza kwa kusema “ Mradi wa maji vijijini na Mijini ni sehemu ya Ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi, na Mafanikio haya ni utekelezaji wa Serikali unaoongozwa chini ya Chama cha Mapinduzi. Hivyo aliwaasa Wananchi wote wa kata ya Lilambo pamoja na viongozi kutumia muda wao kuelezea mafanikio yote yaliyofanywa na Mh. Rais DR John Pombe Magufuli.
Homera alisema Kata ya Lilambo kwa sasa haina shida tena ya Maji safi kama ilivyokuwa awali kutokana na huduma hiyo kupatikana kwa ukaribu na kwa uhakika bila usumbufu wowote.
Naye Meneja wa Ufundi Souwasa Jafari Yahaya alibainisha kuwa, Kutokana na mabadiliko ya Sheria ya usimamizi wa huduma za maji safi na mazingira, Mkataba wa Mradi huo ulihamishiwa kutoka kwa Wakala wa Maji safi na Mazingira Vijijini (RUWASA) na kwenda Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA).
Yahaya Alizitaja kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa visima (ring wells), ujenzi wa Tanki la Sump meta za ujazo 25, usambazaji na ufungaji wa pampu na transfoma ya umeme, pamoja na kupima uwingi wa maji katika chanzo, ujenzi wa kibanda cha mashine.
Aliongeza kuwa kazi nyingine zilizofanyika ili kukamilisha mradi huo ni pamoja na ujenzi wa uzio meta 160, usambazaji, na uchimbaji wa mitaro na ulazaji bomba, ujenzi wa vituo 18 vya maji, ujenzi wa chemba 4 za kufungia maji, ujenzi wa tanki la lita 150,000, pamoja na tanki la kutibu maji kwa kutumia klorin( calcium hypochlorite).
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KAIMU AFISA HABARI-MANISPAA YA SONGEA
09/07/2020.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa