Na John Stephen
Wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameadhimisha siku ya Homa ya Ini duniani kwa kutoa huduma ya upimaji wa afya kwa watu 375, huku 29 kati yao wakiwa wameambukizwa ugonjwa wa Homa ya Ini na 55 wakiwa wamepatiwa chanjo.
MNH imetoa huduma ya kupima watu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya Homa ya Ini duniani ambayo hufanyika tarehe 28 Julai kila mwaka.
Kati ya watu 375 waliojitokeza wanaume ni 175 na wanawake ni 200 ambapo watu 346 hawana ugonjwa wa Homa ya Ini.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini wa Muhimbili, Dkt. Masolwa Ng’wanasayi amesema watu waliobainika kuwa na Homa ya Ini wameshauriwa kwenda hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Dkt. Ng’wanasayi amesema lengo la kufanya uchunguzi wa afya kwa watu mbalimbali ni kuongeza uelewa katika jamii kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini wa aina ya Hepatitis B.
Mtaalamu amebainisha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu 325 milioni duniani wanaishi na maambukizi ya Homa ya Ini na kwamba asilimia nane ya wakazi wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara wameambukizwa Homa ya Ini aina ya Hepatitis B.
“Hapa kwetu tafiti zinaonyesha asilimia 4.9 wameambukizwa ugonjwa wa Homa ya Ini aina ya Hepatitis B na asilimia 2 wameambukizwa Homa ya Ini aina ya Hepatitis C,” amesema Dkt. Ng’wanasayi.
Amesema kundi la watu wanaotumia dawa za kulevya ni miongoni mwa watu ambao wameambukizwa Homa ya Ini. “Tafiti zinaonyesha kwamba miongoni mwao asilimia 67 hadi 70 wameambukizwa Homa ya Ini,” amesema.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa