MKURUGENZI wa TEHAMA wa Wizara ya Afya Haji Bamsi ameshauri kutumia tovuti za hospitali zilizoanzishwa kutangaza kazi kubwa ya kuokoa maisha inayofanywa na hospitali.
Bamsi alikuwa anazungumza katika mafunzo ya siku tano ya utengenezaji wa tovuti za hospitali kwa maafisa TEHAMA wa hospitali za rufaa za mikoa na hospitali tano za Halmashauri za wilaya yaliyofanyika mjini Morogoro.
Amesema kuna mambo mengi ambayo yanafanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya lakini hayapati nafasi ya kutangazwa katika vyombo vya habari.
Amesema vyombo vingi vya habari vimekuwa vinatangaza habari mbaya zaidi zinazotokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuacha habari nzuri zinaweza kuleta matokeo makubwa kwa wananchi
“Tovuti hizi za hospitali zisaidie kutangaza mambo mazuri mengi yanayofanywa na hospitali ili yaweze kufahamika kwa wananchi ikiwemo kutoa elimu kwa umma katika masuala mbalimbali ya afya’’,alisema.
Bamsi amesema kuna habari nyingi ambazo zinaendelea katika hospitali ikiwemo miradi mbalimbali ya afya,elimu ya magonjwa mbalimbali,kuelimisha kuhusu Bima ya Afya na CHF iliyoboreshwa ambazo hazipati nafasi ya kutangazwa katika vyombo vya habari.
Amesema tovuti zilizoanzishwa zikitumika vizuri zitasaidia wananchi wengi kupata taarifa nyingi za afya ambazo pia zinaweza kusambazwa katika mitandao ya kihabari kutoka katika tovuti na kuwafikia wananchi wengi.
“Hatutaki kusubiri kutangaza habari za hospitali kwa matukio mfano kuzaliwa watoto hadi siku za sikukuu ndiyo zinatangazwa,wakati hopsitali zinafanyakazi kubwa ya kuzalisha watoto na kuokoa maisha ya watu kila siku’’,anasisitiza.
Mafunzo ya utengenezaji tovuti za hospitali yameratibiwa na TAMISEMI na kuwashirikisha maafisa TEHAMA 65 kutoka katika hospitali za Rufaa za mikoa 28 na maafisa TEHAMA watano kutoka katika hospitali tano za Halmashauri nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Septemba 30,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa