Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, amewataka watumishi wa Manispaa ya Songea kutii mamlaka ya viongozi wao, akinukuu maandiko ya Biblia kutoka Warumi 13.
Wakili Muhoja aliyasema haya wakati wa kufunga tamasha la michezo lililofanyika leo, tarehe 9 Novemba 2024, katika uwanja wa Majimaji.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Wakili Muhoja alimtaka Afisa Michezo wa Manispaa ya Songea, Mohamed Kites, kuunda kikundi cha kufanya mazoezi, ambacho kitajumuisha watu kati ya 40 hadi 50. Kikundi hicho kitakuwa kinafanya mazoezi kila Jumanne, Alhamisi, na Jumamosi kuanzia saa 12 asubuhi kabla ya kuendelea na majukumu ya kazi. Alisema, "Ni muhimu kwa watumishi wetu kuwa na afya bora ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi."
Aidha, Wakili Muhoja alizitaka taasisi mbalimbali kushirikiana na kuendelea kujitokeza kuimarisha afya na kudumisha ushirikiano katika kulitumikia taifa letu, Aidha, Aliendelea kusisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya bora na msingi kwa jamii.
Katika hatua nyingine, aliahidi kukutana na walimu wa michezo katika shule mbalimbali ili kuandaa vijana kwa michezo ijayo, akisema kuwa maandalizi bora ndiyo ufunguo wa mafanikio. Alisisitiza kuwa "kila kitu kizuri kina maandalizi yake."
Pia, alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwatakia heri wanafunzi wanaojiandaa kufanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2024, ambao unatarajiwa kuanza tarehe 11 Novemba 2024.
Tamasha la michezo lililofanyika leo lilikuwa ni mwendelezo wa shughuli za kila mwezi za kufanya mazoezi ya viungo, ambazo hufanyika katika wiki ya mwanzo wa kila mwezi.
Imeandaliwa na:
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa