Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma zao kwa ustadi na kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari na wadau mbalimbali yaliyofanyika katika ukumbi wa HOMSO tarehe 19 Novemba 2024 na kuendeshwa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kanali Ahmed aliwasihi waandishi kutii misingi ya maadili ili kutoa habari zilizo sahihii.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa rai kwa viongozi wa chama hicho kuendelea kuwahimiza waandishi wanaokwenda kinyume na maadili ya tasnia ya uandishi wa habari, ili waonyeshwe njia sahihi ya kuandika na kutekeleza jukumu lao.
Alisema kuwa ni muhimu kwa waandishi kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kwa wingi katika upigaji kura, hususan katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Wakili Dickson Ndunguru, ambaye ni wakili wa kujitegemea, alizungumzia umuhimu wa uhuru wa kujieleza na kusema kwamba ni haki ya kila mtu au jamii kueleza mawazo na maoni yao.
Alisisitiza kuwa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa kujieleza, huku akieleza kuwa sheria nyingine kama vile sheria ya magazeti, usalama, na msaada wa habari zinahitaji kuzingatiwa ili kuhakikisha uhuru huu unatumika ipasavyo.
Aliongeza kuwa uhuru wa kujieleza ni muhimu kwa jamii katika kukuza uwajibikaji na maendeleo.
Kwa upande mwingine, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Shekhe Ramadhani Mwakilima, alitoa maoni yake kuhusu uhuru wa kujieleza kutoka katika mtazamo wa kidini ambapo alisisitiza kuwa dini haitoi kikwazo kwa mtu kujieleza, lakini inasisitiza kwamba kila mtu anapaswa kutumia uhuru wake kwa njia inayojenga umoja na si kutenganisha jamii.
Mafunzo haya, yaliyojumuisha waandishi wa habari na wadau mbalimbali, yalilenga kukuza na kuimarisha uhuru wa kujieleza, huku wakihimiza umuhimu wa maadili na sheria katika tasnia ya habari.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa