Katibu tawala Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Damas Dominic Suta, amewataka watumishi katika mkoa huo kujiunga na vyama vya wafanyakazi, akisisitiza kuwa sheria ya ajira na mahusiano kazini inawataka watumishi ambao si wanachama wa vyama vya wafanyakazi kulipa ada ya uwakala ambapo Hii ni kutokana na ukweli kwamba vyama vya wafanyakazi vinapodai haki za watumishi, hata wale wasiokuwa wanachama, wanapata faida ya huduma hizo.
Dkt. Suta alisema kuwa chama cha wafanyakazi kinaweza kupata hati ya usajili lakini kisitambulike rasmi na Serikali, na ili chama hicho kitambulike na Serikali, kinahitaji kuwa na usajili halali na kuwa na wanachama wengi zaidi kuliko vyama vingine, pamoja na kuhakikisha kinawakilisha maslahi ya wanachama, hata wale wasio wanachama.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kusimama imara katika kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi ambapo Alisisitiza kuwa mara tu wanapopokea changamoto zinazohusu masuala ya utumishi, viongozi wanapaswa kufika kwa viongozi wa ngazi za juu ili kupata ufafanuzi na kutatua matatizo hayo kwa haraka.
Katika hatua nyingine, Dkt. Suta alitoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Idara za Ardhi kuhakikisha wanatenga bajeti ya kutosha inayotokana na mapato ya ndani ili huduma zinazotolewa na idara hiyo ziweze kufanywa kwa ufanisi na kwa viwango vinavyostahili.
Hayo yalisemwa na Dkt. Suta katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika tarehe 12 Novemba 2024 katika ukumbi wa Hazina Ndogo, Manispaa ya Songea ambapo Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wa kamati ya utendaji wa TALGWU Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Ruvuma, Wiley Luambano, alieleza kuwa mkoa wa Ruvuma unajivunia kuwa na wanachama 4,500 wa TALGWU wasiokuwa walimu huku akisisitiza kuhusu madai mbalimbali ya watumishi yasiyohusiana na mishahara, ikiwemo masuala ya uhamisho na likizo.
Mwenyekiti Luambano pia alitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuajiri watumishi 315 katika sekta ya afya, ambao tayari wameanza kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.
IMEANDALIWA NA:
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa