MSHAURI na Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini Tanzania,Kari Leppanen amefanya ziara Mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma. Akihojiwa kwenye Hoteli ya kitalii ya watawa wa Mtakatifu Vincent iliyopo katika fukwe za Kilosa mjini Mbambabay, amesema ameshangazwa na vivutio vya kipekee na adimu ambavyo havipatikani sehemu nyingine yoyote Duniani vilivyopo katika ziwa hilo.
Amesisitiza kuwa iwapo vivutio hivyo vikiendelezwa vitafungua fursa za uwekezaji na utalii kwa wananchi wa eneo hilo na mkoa wa Ruvuma. Miongoni mwa vivutio vilivyopo katika ziwa Nyasa ni fukwe za asili,visiwa ambavyo wanazaliana kwa wingi samaki wa mapambo aina zaidi ya 400, milima ya Livingstone, mawe ya ajabu kama jiwe la Pomonda na vivutio vingine vya Ikolojia na Utamaduni.
Fukwe zilizopo ziwa Nyasa upande wa Tanzania ni miongoni mwa vitega uchumi vizuri na vinavyoweza kuingiza fedha nyingi za kigeni endapo serikali itaamua kusimamia sekta hiyo muhimu ya utalii.
Utafiti ambao umefanywa katika fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania na ziwa Nyasa upande wa Malawi umebaini kuwa fukwe za Tanzania ni bora zaidi kwa kuwa ni za asili ambazo zimetengenezwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
Fukwe za ziwa Nyasa upande wa Malawi zimetengenezwa toka kingo za milima hivyo zimechimbwa hali ambayo inadhihirisha ubora wake hauwezi kulingana na fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania.Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imejaliwa fukwe za asili ambazo zinaaminika kuwa hazifanani na fukwe nyingine zozote duniani na endapo zitaendelezwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato katika wilaya ya Nyasa.
Sekta ya utalii ni kati ya maeneo matatu ya kwanza yanayoliingizia taifa za fedha za kigeni. Hivyo ni wakati muafaka kwa sekta ya utalii kuhakikisha inafanya juhudi za makusudi ili kuwekeza na kulinda fukwe zilizopo katika maziwa na bahari,ambazo zinaweza kuchangia maendeleo katika sekta ya utalii.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Septemba 16,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa