Na;
Amina Pilly;
Afisa Habari.
Serikali za Mitaa ni vyombo vilivyoanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 145 na 146 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja marekebisho yake ambayo majukumu na muundo wa Mamlaka za Serikali za Mitaaa yameainishwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) sura ya 287 na sheria ya Serikali za Mitaa za mamlaka ya Miji sura 288.
Lengo la Mwongozo huo ni kuwawezesha Madiwani na Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuelewa taratibu muhimu za uitishaji na uendeshaji wa mikutano ya kwanza ya Halmashauri baada ya uchaguzi Mkuu.
Hayo yamebainishwa leo 27 Agosti 2022 katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea uliohudhuriwa na wananchi, wataalamu, na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kumthibitisha Naibu Meya na kuunda kamati za kudumu pamoja na kupokea taarifa ya mwaka.
Mstahiki Meya Manispaa ya songea Michael Mbano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amewataka Madiwani kuzingatia agenda zilizopo katika kikao hicho ili kupanga mikakati endelevu kwa maendeleo ya Taifa.
Mhe. Mbano amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha zoezi la kuwapanga wamachinga katika maeneo yaliyotengwa rasmi kwa kufanyia biashara hizo. Sambamba na pongezi hizo ametoa Rai kwa wataalamu hao kuendelea kufanya kazi kwa weredi ikiwemo na kuwa na tabia ya kutembelea miradi mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto au malalamiko ya wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kwa mujibu wa miongozo na kanuni Naibu Meya atatangazwa kuwa amechaguliwa endapo atakuwa amepata zaidi ya nusu ½ ya kura zilizopigwa.
Dkt. Sagamiko aliongeza kuwa iwapo wakati wa kumchagua Naibu Meya kutakuwa na jina moja tu ambalo litakuwa limependekezwa, wajumbe watapiga kura za siri za “ndiyo” endapo zitazidi asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa basi mgombea atatangazwa kuwa Naibu Meya na iwapo kura za hapana zitazidi asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa, jina la mgombea mwingine litapendekezwa kwa njia na utaratibu uliotumika hapo awali.
Aidha baada ya kusoma mwogozo huo hatua za uchaguzi wa kumpigia kura mgombea Jeremia Mlembe ambaye hakuwa na mpinzani uliendelea kufanyika na kwa kupigiwa kura na wajumbe ambao ni waheshimiwa madiwani 28 ambapo kura zilizopigwa ni 27, kura zilizoharibika 0, kura zilizokataliwa ni 0, na kura za ndiyo ni 27 ambapo baada ya matokeo hayo katibu wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Songea kwa mamlaka aliyopewa alimtangaza Mhe. Jeremiah Mlembe Diwani wa Kata ya Bombambili kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Songea.
Baada ya kukamilisha kusimamia zoezi la kumthibitisha Naibu Meya, aliziitambulisha kamati mbalimbali za kudumu za halmashauri ikiwemo na kamati ya fedha, kamati ya mipango miji, kamati ya uchumi na kamati ya maadili na kisha alisoma taarifa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mwaka mmoja 2021 hadi 2022.
Naye Naibu Meya Jeremiah Mlembe alitoa shukrani kwa wajumbe wote waliomchagua nakuahidi kutoa ushirikiano baina ya Waheshimiwa Madiwani na wataalam.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa