Benki ya NMB tawi la Songea imetoa msaada wa madawati, meza, kabati na bati kwa shule za Msingi tatu 3 za Manispaa ya Songea yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 12.
Msaada huo umetolewa jana tarehe 11 machi 2021 kwa shule ya Msingi Legele ambapo walipata bati 60, Shule ya Msingi Mshangano kati walipata madawati 80 pamoja na shule ya Msingi Chandamali walipata viti na meza na kabati kwa ajili ya matumizi ya ofisi za walimu.
Mgeni rasmi katika zoezi hilo la ugawaji wa vifaa vya shule ni mkuu wa Wilaya ya Songea ambaye aliwakilishwa na katibu Tawala Wilaya ya Songea Bi Pendo Daniel ambaye alianza kwa kutoa shukrani kwa Benki ya NMB kwa utamaduni walionao wa kutoa msaada kwa jamii mara kwa mara ambayo ni 1% ya faida wanayoipata kutoka kwa wateja wao.
Bi Pendo amewataka wadau wengine kuwa na desturi ya kusaidia jamii kama wafanyavyo wadau wa Benki NMB kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuchangia huduma bora za Afya, Elimu bure na za kijamii.
Ametoa Rai kwa jamii kuhamasika kwa wingi kufungua akaunti Benki ya NMB ili waweze kutoa msaada zaidi kwa jamii.
Naye Meneja wa kanda wa Benk NMB Janeth Shango alisema lengo la NMB ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano ambayo inahakikisha inatoa huduma bora za afya, Elimu na huduma nyingine za kijamii.
Shango alisema NMB wanao wajibu wa kushirikiana na Serikali ili kuweza kutatua changamoto ambazo zinapatikana katika maeneo ya kijamii ambapo imejikita kusaidia katika sehemu ya Elimu ambapo huchangia baadhi ya mahitaji ikiwemo na madawati kwa shule za msingi, viti na meza kwa shule za sekondari pamoja na sekta ya Afya husaidia vitanda na magodoro pamoja na bati za kuezekea majengo mbalimbali.
Alisema NMB imekuwa na utamaduni wa kurudisha faida kwa jamii ambayo inaipata katika jamii ambayo inaizunguka kwa kutoa msaada ambao unatokana na 1% ya faida waipatayo kutoka kwa wateja wao kwa kutokana na desturi hiyo, Benki ya NMB mwaka 2020 imefanya vizuri katika soko kwa masuala ya kibenki na imetengeneza kiwango kipya cha upatikanaji wa faida nchini.
Aidha, kupitia huduma hizo Benki ya NMB imekuwa bora kwa miaka 8 nane mfululizo na ndani ya muda huo wamekuwa wakiendelea kutoa 1% ya faida wanayoipata kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii.
Naye afisa Elimu Msingi Manispaa ya Songea Zakia Fandey alitoa shukrani kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa na kisha alisema Halmashauri ina jumla ya shule za msingi 92 kati ya hizo shule tatu 3 zimepokea msaada wa madawati, bati, kabati, viti na meza kutoka Benki ya NMB ambapo amewataka walimu wa shule hizo kuhakikisha wanatunza vizuri vizuri ili viweze kumudu kwa muda mrefu.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
12.03.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa