KAMPUNI ya serikali ya China inayoitwa China Sichuan International Cooperation imesaini mkataba wa miezi 18 na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kujenga stendi mpya ya mabasi katika eneo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mhandisi Samwel Sanya amesema Kampuni hiyo imesaini mkataba ambao unaanzia Machi 25 hadi Septemba 30,2019.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni sita zitatumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa na kwamba ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji,Manispaa iliamua kutenga eneo la kituo kikuu cha mabasi kuwa katika Mtaa wa Tanga ikiwa ni umbali wa takribani kilometa 14 toka mjini Songea.
“Fedha za mradi wa stendi zimetolewa kupitia Benki ya Dunia,jumla ya hekari 29 zimetwaliwa katika eneo hilo ili kupitisha stendi ambapo hekari 20 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 32 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi’’,anasema Mhandisi Sanya.
Kampuni ya China Sichuan International Cooperation imesaini pia mkataba wa miezi 18 wa ukarabati wa barabara za lami nzito katika manispaa ya Songea zenye urefu wa kilometa 10.3,kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni kumi.
Fedha za miradi hiyo ya barabara na stendi zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Machi 23,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa