Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa katika ziara yake nchini pamoja na mambo mengine amekuwa anasisitiza kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji vilivyopo.
Akiwa katika Mkoa wa Ruvuma Majaliwa aliagiza kuwekwa mikakati ya kudhibiti uharibifu wa mazingira na ukataji miti hovyo,akisisitiza kuwa matukio hayo hayana budi kudhibitiwa kabisa kwani yanaweza kuhatarisha kuendelea kuwepo kwa vyanzo vya maji vilivyopo.
“Sote tunafahamu kwamba ili kuendelea kuwa na maji ya uhakika ni lazima kuwa na misitu iliyotunzwa, hivyo,Uongozi wa Halmashauri simamieni kikamilifu sheria ndogo za utunzaji wa mazingira na kuchukua hatua kali wa kwa wote wanaozivunja ’’,anasisitiza Waziri Mkuu katika majumuisho ya ziara yake mkoani Ruvuma.
Sheria ya mazingira inaelekeza wazi kuwa hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya vyanzo vya maji,hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuelimishwa umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kupiga marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo.
Akiwa katika ziara ya Mkoa wa Lindi,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya wakazi wa Ruangwa wanaokata miti kwenye misitu waache kufanya hivyo mara moja ili kuokoa ardhi chepechepe waliyokuwa nayo.
“Zamani kuna maeneo ulikuwa haupiti hadi ukunje suruali, na kama una gari napo pia ilikuwa ni taabu kupita kwenye maeneo hayo. Lakini sasa hivi, hakuna tena maeneo hayo ndiyo maana kila unakopita unakuta akinamama wanatembea mwendo mrefu,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa.
Waziri Mkuu amesema hivi sasa Serikali inatumia gharama kubwa kuchimba visima virefu kutafuta maji,ambapo zamani walikuwa wanachimba mita 20 au 30 wanakuta maji kwa gharama ya sh. milioni 35, na kwamba sasa wanalazimika kuchimba mita zaidi ya 150 kwa gharama ya sh. milioni 75 kwa kisima kimoja.
Bila maji hakuna maisha na ili maji yapatikane lazima vyanzo vya maji vilindwe.Hata hivyo bado tafsiri ya chanzo cha maji kina utata kisheria kwa kuangalia sheria ya mazingira na sheria ya maji.
Ukiangalia sheria ya Maji ya Mwaka 2002 na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004,utabaini kuwa Sheria zote hizi zina vipengele vya utunzaji au kuhifadhi vyanzo vya maji.
Sheria ya Maji hairuhusu kufanyika shughuli za kudumu za binadamu katika mita 200 kutoka mto au vijito na mita 500 kutoka kwenye maziwa au Bahari.
Hata hivyo,sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika kipengele cha 57(1) hairuhusu kazi za kudumu za binadamu kufanyika kwenye maeneo ya vianzio vya maji mita 60.
Shirika la Afya Duniani WHO linasema zaidi ya watu milioni tano hufa kutokana magonjwa yatokanayo na maji kila mwaka ambayo ni mara kumi ya idadi ya watu wanaokufa kutokana na vita.Mamilioni ya watu duniani hutegemea maji ili waishi, na kukosekana kwake husababisha vifo .
Kwa mujibu wa WHO,watu bilioni 1.3 ambao ni moja ya tano ya watu wote duniani wanakosa maji salama ya kunywa kutokana na uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Sera na sheria za utunzaji wa mazingira zipo, kinachotakiwa ni kuhakikisha sheria hizo zinachukua nafasi yake kwa wale wote watakaobainika wanachafua na kuharibu vyanzo vya maji wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Mwandishi wa Makala haya anaitwa Albano Midelo baruapepe:albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa