UJENZI wa barabara ya lami katika kiwango cha lami nzito,unaanza mara moja ambapo serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 67 toka Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ambayo itagharimu shilingi bilioni 129.
Mkataba huo wa miezi 24 umesainiwa Desemba 11,2017 na Kampuni ya Mkandarasi inayoitwa China Henan International Corparation Group Ltd(CHICO) ambayo inatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020.
Tukio la kusaini Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay pamoja na mikataba mingine mitatu ya ujenzi limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa,Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) Marie,Hellen Minja,Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) na Mbunge wa Nyasa na Naibu Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya.
Akizungumza katika Hafla hiyo Mhandisi Manyanya amesema kukamilika kwa barabara hiyo kunafungua milango ya utalii katika mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna karibu aina zote za vivutio vya utalii na uwekezaji na kwamba barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu cha nchi za Tanzania,Malawi na Msumbiji ambazo zitatumia bandari ya Mbambabay.
Kukamilika kwa kipande cha barabara toka Mbinga hadi Nyasa kunakamilisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika ukanda wa Mtwara Corridor toka Mtwara hadi Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma hivyo kufungua milango ya uwekezaji katika ukanda wa kusini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Ruvuma.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa