Manispaa ya Songea inakabiliwa na changamoto ya wazazi ya kutochangia chakula shuleni, jambo ambalo linaathiri uhudhurio wa wanafunzi katika masomo yao ambapo Hali hii ilielezwa na Afisa Elimu wa Manispaa, Bi. Janeth Moyo, katika kikao cha Lishe kilichofanyika leo, tarehe 24 Oktoba 2024, katika ukumbi wa Manispaa.
Bi. Moyo alisema kuwa wazazi na walezi wengi bado hawachangii chakula shuleni, hali inayosababisha wanafunzi wengi kutohudhuria masomo ipasavyo. Ili kukabiliana na hali hii, Manispaa ya Songea imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na kutunga sheria ndogo zitakazosaidia kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wakati wa masomo. Aidha, shule mbili ambazo bado hazijaanzisha klabu za lishe zitaanzishwa.
Afisa Lishe wa Manispaa, Frolentine Kisaka, alisisitiza umuhimu wa lishe bora katika kupambana na udumavu na utapiamlo. Alitoa ripoti ya hali ya lishe kwa akina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, ambapo kati ya watoto 40,283 waliochunguzwa, asilimia 99.69 waligundulika kuwa hawana utapiamlo. Hata hivyo, watoto 19 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali na walipatiwa rufaa kwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Songea.
Kikao hiki ni sehemu ya tathmini ya hali ya lishe katika Manispaa ya Songea kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024 ambapo Manispaa ya Songea inaendelea na juhudi za kuboresha lishe kwa kuhakikisha wazazi wanashiriki kikamilifu katika michango ya chakula shuleni, ili kusaidia wanafunzi kupata chakula bora na kuhudhuria masomo yao kwa ufanisi.
Na,
Amina Pilly;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa