CHANJO mpya ya HIV ambayo ina uwezo wa kuwalinda watu duniani kutokana na virusi hivyo imeonesha matumaini makubwa.Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,tiba hiyo inayolenga kutoa kinga dhidi ya virusi kadhaa, ilitoa kinga ya HIV katika majaribio yaliofanyiwa watu 339, kulingana na utafiti mmoja uliochapishwa katika jarida la Lancet.
Pia iliwalinda tumbili dhidi ya virusi vinavyofanana na HIV.Majaribio zaidi sasa yanafaa kufanywa kubaini iwapo kinga iliotolewa inaweza kuwalinda watu dhidi ya maambukizi ya HIV.
Takriban watu milioni 37 duniani wanaishi na virusi vya ya HIV au Aids na kuna takriban visa vipya milioni 1.8 kila mwaka.Lakini licha ya kupiga hatua dhidi ya HIV , tiba yake na chanjo haijapatikana.
Dawa kwa jina Prep ni nzuri katika kuzuia maambukizi ya HIV lakini ikilinganishwa na chanjo inafaa kutumiwa mara kwa mara, hata kila siku ili kuzuia virusi hivyo kuzaana .Uvumbuzi wa chanjo yake umekuwa changamoto kubwa kwa wanasayansi , kwa sababu kuna aina nyingi za virusi vyake vinavyopatikana katika maeneo kadhaa ya dunia.
Lakini kwa chanjo hii wanasayansi wameweza kutengeneza vipande vya tiba vinayoendana na aina tofauti za virusi vya HIV.Matumaini ni kwamba inaweza kutoa kinga bora zaidi dhidi ya aina tofauti za virusi vya HIV vinavyopatikana katika maeneo mbali mbali ya dunia.Washirika hao kutoka Marekani, Uganda, Afrika Kusini na Thailand walipewa chanjo nne katika kipindi cha wiki 48.
Mchanganyiko wa chanjo hizo ulisababisha kutokea kwa kinga ya HIV na wakaonekana wako salama.Wanasayansi pia waliwafanyia utafiti kama huo tumbili ambao hawana maambukizi ya HIV ili kuwalinda dhidi ya kuambukizwa virusi vinavyofanana na HIV.Chanjo hiyo ilionyesha kwa inaweza kuwalinda asilimia 67 ya tumbili 72 kutopata ugonjwa huo.
Wanasayansi waliwafanyia majaribio watu walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 50 ambao hawakuwa na HIV na walikuwa na afya.''Matokeo haya yanawakilisha hatua kubwa iliopigwa'', alisema Dan Barouch , Profesa wa matibabu katika chuo kikuu cha matibabu cha Havard na kiongozi wa utafiti huo.Hata hivyo Profesa Barouch pia ametahadharisha kwamba matokeo hayo yanafaa kuchanganuliwa na tahadhari.
Ijapokuwa chanjo hiyo ilifanikiwa kuimarisha kinga ya watu waliojitolea kufanya majaribio hayo, haijulikani iwapo itatosha kukabiliana na virusi hivyo na kuzuia maambukizi.''Changamoto katika kutengeza chanjo ya HIV ni nyingi, na uwezo wa kuziimarisha kinga haimaanishi kwamba chanjo hiyo itawalinda binaadamu dhidi ya maambukizi ya HIV'', aliongezea.
Chanzo ni Idhaa ya Kiswahili ya BBC-LONDON
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa