CHUO cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC) kilichopo katika Kijiji cha Likuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kimefanya mahafali ya mafunzo kwa Askari wanyamapori wa vijiji (VGS) ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu.
Akizungumza katika mahafali hayo Naibu Waziri Kanyasu amewaasa askari wahitimu kwenda kuzilinda na kuzitunza rasilimali za taifa katika maeneo yao ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kanyasu ameahidi kushughulikia changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo miundombinu chakavu na kumalizia jengo la maktaba ambalo Naibu Waziri huyo ameweka jiwe msingi na kwamba amesema serikali itahakikisha kuwa chuo hicho kinakuwa na sifa za chuo cha kati.
Awali akizungumza kabla ya mgeni rasmi Mkuu wa chuo cha (CBCTC) Jane Nyau amesema chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1995 ni Chuo pekee cha utoaji wa mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii barani Afrika na kwamba hapa nchini katika vyuo vya uhifadhi ,hakuna chuo kinachotoa mafunzo yanayofanana na chuo hiki,hali hiyo ndiyo inakifanya kuwa ni chuo cha kipekee nchini.
Amesema katika mahafali ya kozi namba 64/2019 ya Askari wanyamapori wa vijiji(VGS) jumla ya wanachuo 20 wamehitimu mafunzo ya Askari wanyamapori wa vijiji (VGS) kwa miezi mitatu.
Nyau amesema licha ya chuo hicho kutoa kozi za mafunzo ya Askari wanyamapori wa vijiji(VGS) ya miezi mitatu na mafunzo ya viongozi wa serikali na Kamati za maliasili za vijiji ya mwezi mmoja,CBCTC kuanzia Julai 2019 kinatarajia kuanza kutoa kozi ya Astashahada ya Awali ya Waongoza watalii kwa muda wa mwaka mmoja.
“Kozi hii itatolewa ili kuendana na mkakati unaoendelea wa serikali wa kukuza utalii katika Ukanda wa Kusini,mtaala wa kozi hiyo umeshakamilika na tayari umeshathibitishwa na Baraza la Usimamizi wa Vyuo vya Ufundi (NACTE)’anasema Nyau.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Juni 5,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa