WAGENI wanaosoma katika chuo cha mafunzo ya ulinzi Kunduchi jijini Dar es salaam wamefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kujifunzo mambo mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo ulinzi na usalama .
Wageni hao ambao ni maafisa kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa katika Manispaa ya Songea walikutana na mwenyeji wao Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Songea.Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo.
Wakiwa katika ukumbi wa Manispaa ya Songea,maafisa hao walipewa taarifa ya Manispaa ya Songea ikiwemo taarifa ya fedha ambayo inaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 Manispaa imekuwa na bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 39,ambapo mapato ya ndani ni zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Kulingana na taarifa hiyo,Manispaa ya Songea inatekeleza miradi mbalimbali katika Kata zote 21 zilizopo katika Manispaa hiyo na kwamba Manispaa hiyo inatekeleza miradi mikubwa inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwemo ujenzi wa machinjiio ya kisasa uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.2 ,ujenzi wa kituo cha mabasi ya kisasa uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 6.1 na ukarabati wa barabara katika kiwango cha lami nzito zenye urefu wa kilometa 10.3 uliogharimu zaidi ya bilioni 10.
Maafisa hao katika Wilaya ya Songea wanatembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Uwanja wa ndege wa Songea,Shamba la Kahawa la AVIV,kiwanda cha Sausage Peramiho,jengo la kihistoria la Kanisa katoliki la Peramiho na Wakala wa hifadhi ya chakula ya Taifa NFRA.
Kulingana na taarifa ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,maafisa hao wanatarajia kutembelea Mkoa wa Ruvuma katika Wilaya za Mbinga kwa kutembelea kiwanda cha kukoboa kahawa na wilaya ya Nyasa kwa kutembelea fukwe za ziwa Nyasa na kwamba ziara hiyo inatarajia kukamilika Januari 11,2020.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Januari 7,2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa