Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15.02.2022
Halmashauri ya Manispaa ya Songea yatoa eneo la hekari 71 kwa ajili ya ujenzi wa tawi la chuo kikuu cha uhasibu kilichopo Arusha hapo jana Februari 14, 2022 katika eneo la kata ya Tanga lililopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza kabla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge alisema ujenzi wa chuo hicho utasaidia kuleta maendeleo pamoja na kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma.
Aliongeza kuwa eneo hilo ambalo limekaa kimkakati kutokana na kuzungukwa na maeneo muhimu kiuchumi ikiwemo na stendi kuu ya mabasi ya Tanga, machinjio ya kisasa pamoja na Hospitali ya rufaa ya Manispaa ya Songea ambayo inatarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.’Alibainisha’
Ibuge alisema miongoni mwa changamoto zilizopo katika eneo hilo ni pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na mawasiliano ambapo ametoa agizo kwa mamlaka husika kuhakikisha wanatatua changamoto hizo na kupeleka huduma hizo kwenye eneo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt Mwaitete Cairo alitoa shukrani kwa uongozi wa Halmashauri ya Mnaispaa ya Songea pamoja na Mkoa wa Ruvuma kwa kutoa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho ambapo alisema kuwa ujenzi huo utaanza mara moja kwa kuzingatia mfumo wa kutumia ‘force account’ hivyo wananchi wajiandae kupata nafasi za ajira pamoja na kuwekeza miradi mbalimbali ambayo itasaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo binafsi na ya Mkoa kwa ujumla.
Akibainisha kuhusiana na mchakato wa ujenzi wa chuo hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema eneo hilo lipo katika kata ya Tanga, mtaa wa pambazuko ambalo limetolewa bure na Manispaa kwa lengo la kutatua changamoto ya ukosefu wa Taasisi za elimu ya juu katika Mkoa wa Ruvuma.
Aidha, Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano ametoa shukrani kwa uongozi wa chuo cha uhasibu Arusha kwa kukubali kujenga tawi la chuo hicho ambapo wamejibu kilio cha wananchi kuhusu upatikanaji wa Taasisi za elimu ya juu Mkoani Ruvuma.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Hamis Abdallah Ally ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa chuo hicho kama walivyotoa ushirikianokatika utekelezaji wa miradi mingine iliyopo ndani ya kata ya Tanga.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa