HALMASHAURI ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma inatarajia kuanza kutekelela mradi wa kuchakata,kuongeza ubora wa dagaa wanaopatikana ziwa Nyasa na kuwauza ndani na nje ya nchi.
Mradi huo unatarajia kuongeza thamani dagaa hao ambao wanaongoza kwa utamu na ubora lengo likiwa ni kuongeza mapato katika halmashauri,mkoa na Taifa kwa ujumla wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dkt. Oscar Mbyuzi amesema Halmashauri yake inakusudia kuanza kutekeleza mradi wa kuchakata na kuongeza ubora wa dagaa na kufikia soko lililoko nje ya Nchi.
“Halmashauri yetu inatarajia kuongeza ubora wa dagaa kwa kuwakaanga na kuongeza ubora kwa kutumia teknolojia ambayo VETA na SIDO watafundisha na kuweka katika vifungashio vya robo,nusu na kilo moja’’,anasema Dkt.Mbyuzi.
Kulingana na Mkurugenzi huyo,Halmashauri itanunua msimbomilia na kuthibitishwa na Mamlaka ya Uthibiti wa viwango na ubora Tanzania (TBS) ambapo kila robo kilo ya dagaa Nyasa baada ya kuwachakata inatarajiwa kuuzwa kwa kiasi cha shilingi 2500/=
Hata hivyo Mbyuzi amesema mradi huo ambao utafanyika ndani ya Wilaya ya Nyasa unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi billioni moja, ambazo zimeombwa toka Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2018-2019.
Kuanzishwa kwa mradi huo kutaongeza thamani ya dagaa Nyasa hali ambayo itaongeza mapato kwa wananchi na kwamba Halmashauri ya Nyasa itaongeza mapato yake kwa asilimia saba ya mapato yote ya ndani.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini.
Juni 20,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa