Manispaa ya Songea ni miongoni mwa Halmashauri nane 8 zilizopo Mkoani Ruvuma ambazo zinatekeleza zoezi la umezeshaji dawa za minyoo kwa wanafunzi wa shule za msingi 93 zilizopo Manispaa ya Songea ambapo zoezi hilo litaendeshwa na Walimu wa afya chini ya usimamizi wa Wataalamu wa afya linalotarajia kufanyika tarehe 18 machi 2021.
Katika kufanikisha zoezi hilo Manispaa ya Songea imetoa mafunzo kwa walimu wakuu wa shule za Msingi 93, walimu wa afya 93 kutoka kila shule, wenyeviti wa mitaa 95, na watendaji wa kata 21 yaliyofanyika 16 hadi 17 machi 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Manispaa ya Songea Broady Komba alisema jumla ya washiriki wa mafunzo 186 ambao ni walimu wa shule za msingi Manispaa ya Songea wamepewa mafunzo kwa ajili ya kusimamia zoezi la kuwamezesha wanafunzi dawa za kutibu minyoo ya tumbo ambalo linatekelezwa chini ya Wizara ya Afya kwa magonjwa ambayo yamekuwa hayapewi kipaumbele.
Broady alisema mwaka 2021 shule 30 kati ya shule 93 zilizopo Manispaa ya Songea zilifanyiwa utafiti kwa wanafunzi 1548 wa darasa la kwanza na la pili ambao walichukuliwa damu na kupimwa kuangalia kama wanavimelea vya wadudu wa matende na mabusha, na baada ya vipimo kufanyika utafiti ulionyesha kupungua kwa kiasi kikubwa cha vimelea vya wadudu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Alieleza kuwa mwaka 2021 dawa itakayotolewa kwa wanafunzi ni aina moja tu ambayo ni ya dawa Albendazole- dawa za minyoo ya tumbo ambayo humezwa kidonge kimoja tu na unashauriwa kula chakula kabla ya kumeza dawa hiyo.
Aliongeza kuwa dawa za kinga tiba ni salama na hazina madhara endapo zitatumika kwa usahihi japokuwa yapo baadhi ya maudhi madogomadogo yanayoweza kutokea lakini hayana madhara na ni ya muda mfupi ikiwemo na kichefuchefu, kuharisha, kichwa kuuma, homa, na maumivu ya tumbo.
Alisema maudhi haya yanatokana na uwepo wa vimelea vya magonjwa hayo mwilini ambapo unashauriwa kunywa maji mengi, au kutumia dawa za kutuliza maumivu endapo kama zitahitajika. Hivyo amewataka viongozi wa serikali za mitaa kutoa elimu kwa wazazi / wananchi juu ya utoaji wa chakula kwa watoto wao kabla ya kumeza dawa.
Aliongeza kuwa yapo Manufaa ya dawa za kinga tiba endapo zitatumika kwa usahihi ikiwemo na kupunguza maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, kuua vimelea vya magonjwa hayo, kuepusha upungufu wadamu, kupunguza magonjwa ya ngozi, kuboresha nguvu kazi pamoja na kuwafanya watoto wakue vizuri.
Naye mratibu wa Elimu wa Afya Manispaa ya Songea Happiness Shenkunde alisema kwa mwaka 2021 Manispaa ya Songea inatarajia kutoa dawa za minyoo ya tumbo kwa wanafunzi 53962 kati ya wavulana 26758 na wasichana 27204.
Shenkunde amewataka walimu hao kusimamia zoezi hilo kwa weredi na kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu wa Afya na kuhakikisha wanafunzi walioandikishwa wote wenye umri kuanzia miaka 5 hadi 14 wanapewa dawa za kinga tiba.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
17.03.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa