MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,Pololet Mgema amezindua rasmi Bodi ya Huduma za Afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ukiwashirikisha viongozi wa Bodi hiyo,wajumbe na watalaam wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye aliwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mhandisi Samwel Sanya.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa Bodi hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema ameiagiza Bodi hiyo kusimamia dawa za serikali kuhakikisha dawa hizo zinalindwa kwa kuwa ni rasilimali za umma hivyo zinatakiwa kutumika kwa ajili ya wananchi wote.
Bodi ya Huduma za Afya katika Manispaa ya Songea iliteuliwa tangu Novemba 2017 na imekuwa inafanyakazi bila uzinduzi rasmi.
“Mara tu baada ya Bodi kuundwa,ilitakuwa kuzinduliwa na kupewa majukumu rasmi ambayo inatakiwa kutekeleza ya kusimamia huduma za Afya kwa wananchi wetu,leo hii tuna miezi saba tangu Bodi hii iundwe,naamini katika kipindi hiki Bodi ilikuwa inafanya kazi na kufanya vikao’’,anasisitiza Mgema.
Ameshauri wakati mwingine uundaji wa Bodi na uzinduzi wake ufanyike pamoja ili utekelezaji ufanyike kwa ufanisi mkubwa badala ya kufanyika tofauti.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Franco Haule amemthibitishia Mkuu wa wilaya ya Songea kuwa,Bodi itatekeleza maagizo yote kwa vitendo ili kuhakikisha huduma za Afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuanzia ngazi ya zahanati na vituo vya Afya zinatolewa kwa wananchi wote kwa wakati bila upendeleo wowote kwa mujibu wa miongozo na sheria za afya.
Bodi ya Huduma za Afya katika Halmashauri ilianzishwa chini ya kifungu cha nne cha Hati rasmi.Bodi hiyo ambayo inadumu kwa miaka mitatu,inaundwa na Mwenyekiti,Makamu Mwenyekiti,wawakilishi wanne wa watumiaji wa huduma za afya,Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma ya Elimu,Afya na Maji na wataalam wanne toka Halmashauri.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 20,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa