MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Mfaume Kizigo amepishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme Agosti 6 2018 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Hafla fupi ya kuapishwa Kizigo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Wakurugenzi wa Halmashauri,wakuu wa Wilaya,viongozi wa ulinzi na usalama, viongozi wa dini, viongozi wa mila na desturi wa Baraza la Makumbusho ya Taifa ya Majimaji pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo ameahidi kumuwakilisha vema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika Wilaya ya Namtumbo na kwamba atawaletea wananchi maendeleo kwa kuhakikisha anatimiza Irani ya Chama Cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza watendaji na viongozi katika Halmashauri zote mkoani Ruvuma kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 100.
“Chukueni hatua kuwafukuza watumishi ambao hawautakii mema mkoa wa Ruvuma ni aibu mkoa tajiri kama Ruvuma kuwa wa mwisho kimapato swala hili sitalivumilia tena ndani ya mkoa wa Ruvuma na sitolifumbia macho”,amesisitiza Mndeme.
Katika mwaka fedha 2017/2018 Wilaya ya Mbinga na Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma hazikufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato baada ya kushika nafasi za mwisho kitaifa.
Imetolewa na,
Victoria Ndejembi,
wa Kitengo cha TEHAMA Manispaa Songea,
Agosti 7,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa