MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Pololet Mgema amekabidhi mabati 70 yenye thamani ya shilingi milioni 1.82 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Mitendewawa iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mgema pia ameahidi kumalizia mabati mengine 62 kwa ajili ya Ujenzi wa madarasa mawili na Ofisi moja ya shule hiyo.
Katika makabidhiano hayo Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa jukumu la Serikali ni kukamilisha madarasa na miundombinu mingine ya shule,hivyo amewataka Wananchi kuendelea kujenga madarasa ya kutosha kwa ajili ya kupunguza msongamano uliopo.
Katika jitihada za kukamilisha madarasa hayo mawili Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya ukamilishaji wa madarasa hayo mawili.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mitendewawa Aron Mhagama ameeleza kuwa Shule ya Msingi mitendewawa ina wanafunzi 162 ambao ni kuanzia darasa la awali mpaka darasa la nne.
Hata hivyo amesema hadi sasa shule hiyo ina madarasa mawili tu hivyo kufanya msongamano mkubwa wa wanafunzi.
Mhagama amesema mwaka huu wamepanga kukamilisha madarasa mawili na kujenga madarasa mapya matatu na ambapo hadi sasa wamefyatua tofari 40,000 kati ya 80,000 zinazohitajika.
Mwenyekiti huyo wa Mtaa ameiomba Halmashauri ya Manispaa kuongeza madawati kwenye shule hiyo, ombi ambalo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea amelikubali na kuahidi kulifanyia kazi haraka.
Imetolewa na Kitengo cha TEHAMA
Manispaa ya Songea
Julai 13,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa