Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile ameiasa jamii kuwa na uwajibikaji na malezi bora ya watoto wao ili kupunguza au kuondoa ongezeko la watoto wa mtaani.
Alisema ili kuondoa matabaka na unyanyasaji wa kijinsia kwa jamii ni lazima kupambana kuondoa unyonge, na fikra potofu ili kuwa na Usawa na Haki.
Hayo yameinishwa katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kuelekea siku ya kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 08 Machi Duniani kote kwa lengo la kukumbushana juu ya haki, usawa kwa jamii hususani wanawake kushiriki katika kuchangia maendeleo, yaliyofanyika katika uwanja wa Majimaji tarehe 01 Machi 2023.
Ndile alisema lengo ni kutambua nafasi na mchango mwanamke katika kuchangia maendeleo ya jamii ambapo amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kujiunga vikundi vya wajasiliamali ili kuweza kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 10% ili iweze kuwainua kiuchumi na kuongeza pato la familia.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Songea Martin Mtani amesema mikopo ya asilimia 4% ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha wanawake kiuchumi inaendelea kutolewa kila robo ya mwaka kwa lengo la kujenga Tanzania ya viwanda.
Mtani aliongeza kuwa katika kipindi cha julai hadi Deisemba 2023 Manispaa ya Songea imetoa mikopo ya thamani ya Mil. 286,700,000 ambayo ni 10% ya mapato ya ndani iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake.
Akibainisha baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili wanawake ni pamoja na familia kukosa malezi bora kutokana na mvunjiko wa ndoa, mwamko duni wa wanawake katika kufanya shughuli za kiuchumi, pamoja ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu
Ili kukabiliana na changamoto hizo Manispaa ya Songea inaendelea na utoaji wa elimu kwa jamii, wadau, kwa kupitia mikutano ya Serikali za mitaa, vikao mbalimbali, na vyombo vya Habari ili kuweka usawa katika jamii.
KAULI MBIU.
“UBUNIFU NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA”
IMETOLEWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa