Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ameongoza maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ambaye alifariki tarehe 17 machi 2021 na kuzikwa 26 machi 2021 Chato Mkoani Geita.
Maombolezo hayo yamefanyika jana tarehe 27 machi 2021 na kuhudhuriwa na viongozi wa dini, wananchi wa Songea yaliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea ambapo ni siku moja baada ya Baba yetu kulala katika nyumba yake ya milele.
Pololet alisema mnamo tarehe 17.03.2021 saa 5 usiku, aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani alitangaza kutokea kwa kifo cha Rais John Pombe Magufuli na kisha kutangaza siku 21 za maombolezo ya kifo cha kiongozi mkuu wa Taifa letu.
Alisema lengo la kusanyiko hilo lilikuwa kwa ajili ya kuweka kumbukumbu na kufarijiana pamoja na kueleza sifa thabiti alizonazo mwanamapinduzi, mpenda Amani, na mtetezi wa wanyonge Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Alisema Taifa letu limepata msiba mkubwa ambao umetokea na ni kwa mara ya kwanza tumepata msiba wa Rais kufariki akiwa madarakani japo kuwa tumewahi kupata msiba wa Rais wastaafu wawili ambao ni Hayati Mwl Julius Nyerere na Hayati Benjamini Mkapa.
Alisema nanukuu “tunatambua kuwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassani amekuwa na uzoefu mkubwa sana katika shughuli za Serikali kuanzia akiwa mjumbe wa baraza la wakilishi Zanzibar, akiwa Waziri Serikalini kwa nafasi mbalimbali nchini, kuanzia 2015 aliteuliwa na hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mgombea mwenza na hatimaye kuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alifanya kazi na Rais John Pombe Magufuli mpaka umauti ulipomchukua na kwa mujibu wa katiba aliapishwa na kupokea madaraka na kwasasa yeye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Alisema Pololet.
Amewatoa hofu wananchi wa Songea,” amelala mtetezi wa wanyonge lakini yupo jemedali ambaye alikuwa msaidizi wake mkuu ndiye atakwenda kusimamia mipango yote ya utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi”. Alisema Serikali bado ni ileile ambayo ni Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa sita ambaye ni Samia Suluhu Hassani.
Naye mchungaji wa kanisa la KKKT Songea Mjini George Kihegulo alisema “ tunaamini ya kwamba mungu amemuita na tunamuomba mungu ampumzishe kwa Amani mara ya baada ya kulitumikia Taifa hili.
Naye Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Shabani Kitete amewataka wanaruvuma na Taifa kwa ujumla kumkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa mema yote aliyofanya akiwa hai na kuachana na matamshi mabaya kwa Marehemu kwani vitabu vitakatifu vimekataza, hivyo tunapaswa kuendelea kumuombea Dua na Sala ili marehemu apumzike kwa Amani.
Naye Naibu Meya Manispaa ya Songea Jeremia Mirembe amewataka wananchi wote kuendelea kufanya maombolezo hadi 07.04.2021 kama Serikali ilivyotangaza, kupitia hilo ametoa rai kwa wananchi wa Songea kuachana na tabia ya kupiga miziki kwenye kumbi za starehe na meaneo yote ya makazi ya watu bali kwasasa wanapaswa kuweka nyimbo za maombolezo ili kuungana na Serikali katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kifo cha Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
INNALILLAH WAINAILAIHI RAJIUUN. (PUMZIKA KWA AMANI).
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
27. 03.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa