Mwandishi wa Habari raia wa Ufaransa, Raoul Follereau alitumia muda wake mwingi kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma.Kutokana na athari za ugonjwa wa ukoma jamii inatakiwa kuweka kipaumbele kwa kuwapatia huduma stahiki wagonjwa wa ukoma na watu walioathirika na ukoma.
Ugonjwa wa ukoma umekuwa ukiogopwa kutokana na kusababisha ulemavu wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi,ombaomba na kutothaminiwa katika jamii inayowazunguka.Katika Mkoa wa Ruvuma,tangu mwaka 1917 wakoloni waliweka eneo maalum katika kisiwa cha Lundo kilichopo ziwa Nyasa,kwa ajili ya kuwatunza watu waliokuwa na ugonjwa wa ukoma kutokana na ugonjwa huo kusababisha ulemavu wa miguu na mikono hivyo kushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 17duniani ambazo bado zina viwango vya juu vya ugonjwa wa ukoma. Mwaka 2013 Tanzania ilisaini makubaliano katika mkutano uliofanyika Bangkok Thailand yalioazimia kuwa na dunia bila ugonjwa wa ukoma.Miongoni mwa changamoto zinazotajwakuchelewesha kutokomeza ugonjwa wa ukoma ni jamii kuendelea kushikilia imanipotofu juu ya ukoma na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadiwanapopata ulemavu.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu anasisitiza kuwa ukoma bado upo hapa nchini hivyo ni wajibu wa kila mdau kukabiliana nao.Hata hivyo Mwalimu anabainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa huo kutoka kiwango cha utokomezaji cha watu 0.9 kati ya watu 10,000 mwaka 2006 na kufikia kiwango cha watu 0.4 kati ya watu 10,000 mwaka 2015.
“Kwa maana nyingine katika kila watanzania 10,000 kiwango cha watu wenye ugonjwa wa ukoma sasa ni watu 0.4 mwaka 2015 kutoka wastani wa wagonjwa 0.9 katika watu 10,000 mwaka 2015. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa sababu kiwango cha kimataifa cha utokomezaji ukoma kinatakiwa kuwa chini ya mgonjwa mmoja katika watu 10,000’’,anasisitiza Mwalimu.
Anaitaja mikoa na wilaya ambazo zina wagonjwa wengi wa ukoma kuwa ni Lindi (Lindi Manispaa, Liwale, Lindi na Ruangwa),Morogoro (Halmashauri ya Ulanga, Kilombero na Mvomero), Dar es Salaam (Manispaa ya Temeke na Kigamboni) na Tanga ( Halmashauri za Muheza, Mkinga na Pangani).Mikoa mingine ni Mtwara (Halmashauri ya Nanyumbu na Newala),Rukwa (Halmashauri ya Nkasi),Pwani (Halmashauri ya Rufiji na Mkuranga), Geita (Halmashauri ya mji Geita na Halmashauri ya Chato), Tabora (Halmashauri ya Sikonge), Mwanza (Halmashauri ya Kwimba na Misungwi), na Ruvuma (Halmashauri ya Songea na Namtumbo).
Anatoa rai kwa Mikoa na halmashauri hizo kuongeza juhudi za ziada na kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa ukoma kabla ya mwaka 2030 kama yalivyo malengo ya maendeleo endelevu ya dunia.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo
Mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa