EPZA imetenga fedha shilingi Bil. 5.3 kwa ajili ya kulipa fidia kwa Wananchi 955 wa Kata ya Mwengemshindo, kwa lengo la kupisha maeneo yatakayotumika kwa ajili ya uwekezaji wa mradi wa EPZA.
Mamlaka ya EPZA kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Songea iliendesha zoezi la ulipaji wa fidia kwa awamu ya kwanza katika eneo la Mwengemshindo kuanzia tarehe 08/6/2015 hadi tarehe 19/06/2015. Katika zoezi hilo wananchi wapatao 1,183 (kati ya 2,149) walipaswa kulipwa fidia kiasi cha Sh. 1,926,866,730/= baada ya viwango vya fidia kuhuishwa kwa kuongezwa riba ya 8% kwa mujibu wa sheria ambapo hadi kufikia tarehe 19/06/2015 wananchi wapatao 1,130 walichukua hundi zao.
Aidha, kati ya wananchi 1,183 ambao malipo yao yalitayarishwa, wananchi 53 waliostahili kulipwa Sh. 31,215,492 hawakuchukua hundi zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutojitokeza wakati wa zoezi la malipo na wengine kutokamilisha taratibu na nyaraka za mirathi kwa wakati kwa hundi zilizoandikwa kwa jina la marehemu ambao ndiyo walishiriki katika zoezi la uthamini hata hivyo Wananchi 966 hawakulipwa fidia katika awamu ya kwanza ambapo kwa mujibu wa uthamini uliofanyika mwaka 2009 jumla ya fidia yao ilikuwa Tshs. 2,024,319,947, pia Kwa mujibu wa sheria kiwango hiki kinapaswa kuhuishwa kwa kuongezwa riba ambayo inayopaswa kuongezwa (compounding interest) kwa kipindi hiki ni 7%.
Aidha, Wananchi 11 kati ya 966 ambao hawakulipwa fidia awamu ya kwanza, walilipwa mnamo tarehe 01 Februari, 2023 baada ya kuchukua baadhi ya eneo lenye ukubwa wa ekari 300 ndani ya eneo la Ruvuma SEZ kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ambayo inaeendelea kujengwa na kubaki jumla ya Wananchi 955 ndiyo ambao hawajalipwa hadi sasa.
Hayo yamejiri kwenye mkutano wa Wananchi wa kata ya Mwengemshindo wakati wa ufunguzi wa malipo ya fidia ya ardhi, mimea, Nyumba au mashamba uliofanyika tarehe 16 julai 2023 katika ofisi ya kata ya Mwengemshindo ambao ulihudhuriwa na wananchi, EPZA pamoja na wataalamu mbalimbali kwa lengo la kuweka uwazi na usawa katika ulipaji wa fidia kwa wananchi wa kata ya Mwengemshindo.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal. Laban Thomas “ amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro, Diwani wa Kata ya Mwengemshindo pamoja na Vyama vya Siasa kwa usimamizi na ufuatiliaji wa suala hilo ambalo lilikuwa kero kwa wananchi wa kata ya Mwengemshindo.” Alipongeza”
Alisema Malipo haya yalitakiwa kulipwa mwaka 2015 lakini kutokana na kutolipwa kwa wakati malipo hayo yameongezeka kwa asilimia 7% ambayo yatalipwa kwa mwananchi 955 kwa Ekari 5000 ambao tayari wamehakikiwa.
Kanal. Laban amewataka wananchi kutumia vizuri fedha hizo bila kuvunja mahusiano ndani ya familia ambayo yanaweza kusababisha mfarakano katika familia.
Ametoa wito kwa wananchi na wataalamu wa Manispaa ya Songea kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira kila wakati pasipo kusubili usafi wa kila mwisho wa Mwezi ili kuweka mji katika hali ya usafi.
Amewataka wananchi kutoa lishe bora kwa watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na jamii kwa ujumla ili kuwa na jamii yenye afya bora pamoja na kila mwananchi ambaye hajajiunga Mfuko wa Bima ya Afya ahakikishe anajiunga ili kupata matibabu yenye uhakika katika vituo mbalimbali vya afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile alisema” EPZA ni Mamlaka ya maeneo maalumu ya uzalishaji kwa mauzo ya nje ambao huwekeza katika maeneo kwa ajili Uwekezaji wa barabara, na viwanda ambapo Serikali imechukua maeneo ili kujenga viwanda vikubwa vitakavyowezesha kuongeza ajira katika jamii.
Akizungumza mwakilishi wa EPZA Wilson Malosha alisema “ Serikali sasa iko tayari kulipa wananchi ambao hawakulipwa katika wamu ya kwanza ambapo zoezi la uhakiki lilianza tarehe 3 Agosti, 2023 hadi tarehe 10 Agosti ambalo limefanikiwa kupata takwimu sahihi ambapo wananchi 803 kati ya 955 wanaanza kulipwa huku zoezi la uhakiki bado linaendelea ili kukamilisha idadi ya wananchi waliobaki 152 ambao bado hawajahakikiwa.
Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hili la ulipaji ili kila mmoja apate stahili zake na kupisha maeneo kwa ajili ya kuanza uendelezaji ambao utawezesha kupata Wawekezaji kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa wananchi wa kata ya Mwengemshindo wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kufanikiwa kulipa fidia ya ardhi ambayo ilikuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa kata ya Mwengemshindo. “ Wananchi wameshukuru.”
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa