UDANGANYIFU ni tendo lolote la uamuzi au uasi unaofanywa kwa lengo la kuwadanganya wengine na kusababisha anayedanganywa kupata hasara na anayedanganya kufaidika ama kwa kupata fedha.
Akitoa mada ya vihatarishi vya udanganyifu kwa madiwani,wataalam na maafisa watendaji wa mitaa na Kata wa Manispaa ya Songea katika mafunzo ya siku mbili,Mkaguzi wa Ndani wa Manispaa hiyo Joel Mantakara anasema tendo la udanganyifu hujumuisha wizi,rushwa na njama.
Ametahadharisha kuwa hapa nchini mashirika na Taasisi zote zinakabiliwa na hatari za udanganyifu ambapo udanganyifu mkubwa umesababisha kuanguka kwa mashirika katika kufanya biashara.
Mantakara ametolea mfano Kampuni ya kimataifa ya ENRON ambayo ilikuwa inafua umeme huku Taxes nchini Marekani mwaka 2001 Kampuni hiyo ilianguka katika biashara kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na viongozi wa kampuni hiyo katika hesabu zao zikionesha Kampuni inapata faida.
“Viongozi hao walihamasisha wawekezaji waendelee kuwekeza katika Kampuni hiyo wakati katika hali halisi Kampuni ilikuwa inapata hasara katika kiwango cha kutisha hivyo kufikia mwaka 2001Kampuni ilianguka’’,anasema Mantakara.
Anabainisha zaidi kuwa kutokana na udanganyifu,kashfa kubwa zimekuwa zinazikumba Kampuni,Taasisi na mashirika mbalimbali duniani hali ambayo imelazimisha Kampuni zenyewe,mashirika na watu binafsi kuanza kuchukua hatua dhidi ya udanganyifu na ulaghai ili usiendelee kufanyika baada ya kuweka misingi ya kuzuia udanganyifu.
Kwa mujibu wa Mkaguzi huyo wa Ndani wa Manispaa ya Songea,sababu zinazosababisha kuwepo kwa viashiria vya uganganyifu anazitaja kuwa ni mazingira ambayo Taasisi inayafanyia kazi,mfumo wa udhibiti wa ndani na maadili ya Kampuni na maadili ya wafanyakazi.
Hata hivyo Mkaguzi huyo anaeleza kuwa udanganyifu umegawanyika katika maeneo makuu matatu ambayo ni udanganyifu ambao unaweza kufanyika katika taarifa za fedha na udanganyifu unaoweza kufanyika kutokana na matumizi ya rasilimali za Taasisi.
Maeneo mengine ya udanganyifu ni udanganyifu ambao unaweza kufanyika kutokana na rushwa na kukosa maadili na udanganyifu wa ndani ya Taasisi unaohusiana na ajira.
“Mtu yeyote yupo kwenye nafasi ya kuweza kufanya udanganyifu au ulaghai na wakati mwingine watu wanaoweza kufanya ulaghai,wanaweza kuwa katika nafasi kubwa za kazi na wanaheshimika katika jamii na wana maadili mema.wanaweza kuwa viongozi waandamizi,wa kati na wa chini’’,anasisitiza Mantakara.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 2,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa