FUKWE zilizopo ziwa Nyasa upande wa Tanzania ni miongoni mwa vitega uchumi vizuri na vinavyoweza kuingiza fedha nyingi za kigeni endapo serikali itaamua kusimamia sekta hiyo muhimu ya utalii.
Utafiti ambao umefanywa katika fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania na ziwa Nyasa upande wa Malawi umebaini kuwa fukwe za Tanzania ni bora zaidi kwa kuwa ni za asili ambazo zimetengenezwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
Fukwe za ziwa Nyasa upande wa Malawi zimetengenezwa toka kingo za milima hivyo zimechimbwa hali ambayo inadhihirisha ubora wake hauwezi kulingana na fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imejaliwa fukwe za asili ambazo zinaaminika kuwa hazifanani na fukwe nyingine zozote duniani na endapo zitaendelezwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato katika wilaya ya Nyasa.
Jambo la kusitikisha ni kwamba hadi sasa bado juhudi za makusudi hazijaoneshwa na wadau wengi wa utalii kuhakikisha kuwa fukwe zilizopo zinalindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria ili ziwe chanzo cha mapato katika sekta ya utalii.
Ukitembelea katika fukwe za ziwa Nyasa,ni jambo la kawaida kuwakuta wafanyabiashara wanaharibu fukwe hizo kwa kwenda kuchimba mchanga na kuacha mashimo makubwa ambayo yanasababisha uharibifu katika ziwa Nyasa.
Kuna taarifa kuwa baadhi ya fukwe katika ziwa Nyasa zimeuzwa kiholela bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo ujenzi ambao hauzingatii umbali unakubalika kisheria toka katika fukwe hizo.
Hata hivyo Fukwe ya Bayi iliyopo katika eneo la Ndengere Kata ya Mbambabay na fukwe ya Pomonda Kata ya Liuli wilayani Nyasa ndiyo fukwe pekee ambazo zimeanza kuendelezwa na wawekezaji binafsi hivyo kuvutia wageni wengi wanaoingia ziwa Nyasa.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa