Baadhi ya nchi zinazotumia teknolojia ya gesi asilia kwenye magari ni Afrika Kusini, Misri na Msumbiji.Utafiti umebaini kuwa
Matumizi ya mfumo wa gesi asilia katika nchi zilizoanza kutumia umeokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza nishati ya mafuta toka nje ya nchi na kuokoa uharibifu wa mazingira kwa sababu gesi asilia haizalishi hewa ukaa ambayo ni hatari katika mazingira na afya.
Baadhi ya nchi zilizoendelea duniani ikiwemo Norway zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea magari ambapo takwimu zinaonesha kuwa magari yapatayo milioni 11 duniani yanatumia gesi asilia na nchi inayoongoza ni Pakistan yenye magari milioni 2.1, ikifuatiwa na Argentina yenye magari milioni 1.8 Brazil yenye magari milioni 1.7, pamoja na nchi nyingine.
Utafiti ambao umefanywa na wataalam wa gesi asilia unaonesha kuwa gesi asilia ikitumiwa wakati wote, injini ya gari itadumu zaidi kwa sababu haizalishi uchafu ikilinganishwa na petroli na kwamba kama mwenye gari alikuwa anabadili mafuta ya injini kila baada ya kilomita 3,000, mfumo wa kutumia gesi asilia utamwezesha kubadilisha baada ya kilomita 6,000.
Hata hivyo Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Nishati na Madini kuanzia mwaka 1972 hadi 1974, Dk Ben Moshi anakiri kuwa matumizi ya gesi asilia katika huduma mbalimbali nchini, yanaweza kuathiri kampuni nyingi za mafuta zinazofanya biashara hiyo nchini.
Dk. Moshi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi katika Kampuni ya mafuta ya PUMA Energy, anasema kampuni za mafuta nchini hazina budi kukubaliana na mabadiliko yanayokuja kupitia mapinduzi ya nishati ya gesi asilia.
Hapa nchini kulikuwa na mvutano mkali baina ya serikali na wafanyabiashara wa mafuta huku serikali ikituhumu kampuni za mafuta kutengeneza mazingira ya kuhujumu gesi asilia ili isiweze kupoteza soko la mafuta.
Gesi asilia inaweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi ukiachana na matumizi ya gesi kwenye magari,utafiti umebaini gharama ya matumizi ya mkaa na kuni pia inaweza kupungua endapo unatumia gesi asilia kupikia.
Licha ya gesi asilia kutumika kwenye magari,matumizi mengine ya gesi asilia ni kuzalisha umeme ambapo hapa nchini asilimia 70 ya umeme unaozalishwa unatokana na gesi asilia ya Songosongo, uyeyushaji wa vyuma,kwenye viwanda ambapo katika jiji la Dar es salaam viwanda 37 vinatumia gesi asilia na matumizi ya nyumbani.
Kwa mfano ukijaza gesi asilia ya shilingi 64,000 unaweza kutumia kupikia kwa miezi sita,gharama ambayo ni nafuu kwa kuwa jijini Dar es salaam gunia moja la mkaa linauzwa hadi sh.80,000 ambapo familia moja inatumia zaidi ya magunia mawili ya mkaa kwa mwezi.
Gesi asilia ndiyo pekee inayoweza kuinua uchumi kwa haraka kwa kuwa tayari faida kubwa imepatikana tangu kupatikana kwa gesi asilia ya Songosongo ambapo kwa mujibu wa TPDC Taifa limepata dola za Marekani milioni 117.5 kuanzia mwaka 2004 hadi 2012,uchumi umeokoa dola bilioni 4.4 kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2012 .
Imeandikwa na Albano Midelo,mawasiliano 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa