GESI asilia iliyogundulika Tanzania ikisimamiwa vizuri inaweza kuongeza pato la ndani la Taifa (GDP) mara 15 ya pato la sasa hivyo kuifanya Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mtaalamu wa Raslimali za Taifa Kaiza Bubelwa anaishauri Serikali ihakikishe inasimamia vizuri sheria ya gesi asili ili iweze kudhibiti gesi asilia badala ya sekta hiyo kudhibitiwa na wawekezaji.
Anabainisha zaidi kuwa gesi asilia ikidhibitiwa na serikali itaongeza pato la ndani la Taifa mara 15 ya pato la sasa na kwamba makosa ambayo yamefanyika katika sekta ya madini ya kuwanufaisha zaidi wawekezaji kuliko wenye rasilimali yasirudiwe katika gesi asilia na mafuta.
“GDP ya Tanzania mwaka 2011 ilikuwa ni dola za Marekani bilioni 28.5,Kenya ilikuwa ni dola bilioni 34 ambapo gesi asilia pekee ikichimbwa na kusimamiwa inaweza kuongeza uchumi wetu mara 15 ya GDP ya sasa”,anasisitiza Bubelwa.
Bubelwa anasema nchi kwa miaka mingi imeshindwa kunufaika na rasilimali zilizopo kutokana na kukosa usimamizi madhubuti wa rasilimali za madini katika hatua zote za kuanzia utafutaji,uchimbaji,usafirishaji,mikataba na kuweka, sera na sheria zitakazowanufaisha watanzania wote.
Hata hivyo serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli imeonesha nia ya dhati katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa kupitisha sheria za kusimamia rasilimali za nchi ili hatimaye sasa watanzania waweze kunufaika na rasilimali hizo ambazo tumezawadiwa na Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo Bubelwa anataja mambo yaliyochangia watanzania kutonufaika na rasilimali zetu kuwa ni rushwa,upofu wa sheria,ukosefu wa utawala bora, kupotea na kutotumika kwa uwiano katika mfumo wa uchimbaji, maamuzi ya kuchimba na uwazi katika utoaji wa mkataba.
Carlos Mbuta ni Afisa Mkuu Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Mazingira NEMC ametahadharisha kuwa rasilimali ya gesi asilia na mafuta ambayo inachimbwa,siku moja itakwisha hivyo ni lazima kufungua mifuko maalum ya mapato ambayo itatumika kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Gesi asilia inatarajia kuanza kuzalishwa na kusafirishwa mwaka 2021.
Gesi asilia iligundulika kwa mara ya kwanza hapa nchini mwaka 1974 katika kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi,ugunduzi mwingine ulifanyika mkoani Mtwara mwaka 1982 eneo la Mnazibay na ugunduzi bado unaendelea,lakini uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004.
Afisa Mkuu Mwandamizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini TPDC Mhandisi Modesto Lumato anasema jumla ya gesi asilia ambayo imegundulika nchini katika mikoa ya Lindi na Mtwara inafikia futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 ambapo futi trilioni 30 zinatarajiwa kuuzwa nje ya nchi.
Mwanasheria na Mkurugenzi wa Chama cha Watetezi wa Mazingira Tanzania(LEAT) Dk.Nshala Rugemeleza anasisitiza kuwa Tanzania haina wataalamu wa kutosha ambao wanaweza kutuambia ukweli kuhusu madini,gesi na mafuta yaliopo nchini badala yake tunategemea wataalamu kutoka nje ambao wamekuwa wakitoa taarifa za udanganyifu kuhusu rasilimali zetu.
Nchi ya Norway ambayo hivi sasa ina idadi ya watu wasiozidi milioni tano, inapata neema kubwa kutokana na sekta ya mafuta na gesi asilia.Mfuko ulioundwa kwa ajili ya kuweka fedha za rasilimali hizo katika nchi hiyo una zaidi ya Dola za Marekani bilioni 500 ambazo haijulikani zitatumika namna gani kutokana na mfuko kuwa na pesa nyingi.
Kwa uongozi tulionao hivi sasa chini ya Rais Dk.John Magufuli,rasilimali ya gesi asilia inaweza kuiondoa Tanzania katika nchi masikini duniani na kuiingiza kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mwandishi wa Makala haya anaitwa Albano Midelo albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa