UTAFITI umebaini kuwa matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaokoa asilimia 65 ya gharama ukilinganisha na matumizi ya mafuta hali ambayo imesababisha baadhi ya nchi duniani kutumia gesi asilia na kuachana na mafuta.
Baadhi ya nchi duniani zimeanza kutumia gesi asilia kwenye magari hali ambayo imeleta unafuu kwa wananchi na serikali za nchi hizo kutokana na ukweli kuwa gesi asilia kwenye vyombo vya moto ni nafuu ukilinganisha na mafuta.
Baadhi ya nchi ambazo zinazotumia teknolojia ya gesi asilia kwenye magari ni Afrika Kusini,Misri na Msumbiji.
Utafiti umebaini kuwa matumizi ya mfumo wa gesi asilia katika nchi zilizoanza kutumia umeokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza nishati ya mafuta toka nje ya nchi na kuokoa uharibifu wa mazingira kwa sababu gesi asilia haizalishi hewa ukaa ambayo ni hatari katika mazingira na afya.
Baadhi ya nchi zilizoendelea duniani ikiwemo Norway zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea magari ambapo takwimu zinaonesha kuwa magari Zaidi ya milioni 11 duniani yanatumia gesi asilia na nchi inayoongoza ni Pakistan yenye magari milioni 2.1, ikifuatiwa na Argentina yenye magari milioni 1.8 Brazil yenye magari milioni 1.7.
Utafiti ambao umefanywa na wataalam wa gesi asilia unaonesha kuwa gesi asilia ikitumiwa wakati wote, injini ya gari itadumu zaidi kwa sababu haizalishi uchafu ikilinganishwa na petroli na kwamba kama mwenye gari alikuwa anabadili mafuta ya injini kila baada ya kilomita 3,000, mfumo wa kutumia gesi asilia utamwezesha kubadilisha baada ya kilomita 6,000.
Joseph Mkinga Mhandisi ambaye amesomea shahada ya pili ya uhandisi wa mafuta (Petrolium Engineering) nchini Norway anasema nchi ya Norway imepiga hatua kubwa katika sekta ya mafuta na gesi ambapo hivi sasa ni miongoni mwa nchi kumi duniani zinazoongoza kwa uzalishaji wa gesi na mafuta.
Anabainisha kuwa katika nchi ya Norway mabasi yote ya abiria yanatumia gesi asilia badala ya mafuta hali inayosababisha uchumi wa nchi hiyo kukua kwa kasi,serikali yake inasimamia vizuri rasilimali chache zilizopo katika mafuta na gesi asilia hivyo kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu .
Baada ya nchi hiyo kugundua mafuta na gesi,serikali ilianza kuwasomesha vijana wake kuhusu gesi asilia na mafuta na wale wanafunzi wa kwanza waliokuwa wanahitimu waliajiriwa kuwa walimu katika sekta ya gesi na mafuta.
Amesema katika nchi hiyo ambayo hivi sasa inaongoza kwa kuwa na wataalam wengi katika sekta ya mafuta na gesi duniani baadhi yao wanafanyakazi katika nchi ambazo kuna mafuta na gesi ikiwemo Tanzania.
Nchi ya Norway yenye watu wasiozidi milioni tano ilikuwa nchi maskini hadi ilipogundua gesi na mafuta mwaka 1969, ilisimamia sekta hiyo kikamilifu ambapo hivi sasa mfuko wa gesi na mafuta katika nchi hiyo una zaidi ya dola bilioni 500.
Kiasi hicho cha fedha katika nchi ya Norway kitatumika kizazi na kizazi hata kama gesi na mafuta yote katika nchi hiyo yatamalizika.Tanzania inatarajiwa kuwa nchi yenye uchumi wa kati mwaka 2025 baada ya gesi asilia kuanza kuzalishwa rasmi na kuuzwa nje ya nchi.
Kama kweli Tanzania imedhamiria kupata maendeleo makubwa katika sekta ya mafuta na gesi asilia ni vema kuwekeza kwa kuwaandaa wataalam wake kabla ya gesi iliyogundulika kuanza kuzalishwa rasmi.
Hata hivyo juhudi za serikali kuanzisha kozi za mafuta na gesi zimeanza kuonekana baada ya kuanzisha shahada za gesi asilia na mafuta vyuo vikuu vya Dar es salaam na Dodoma tangu mwaka 2014.
Wataalam katika sekta ya gesi asilia na mafuta wakiwepo wa kutosha na serikali kuandaa sera,sheria,miongozo na kanuni bora za sekta ya mafuta na gesi kama ilivyo katika nchi ya Norway sekta hiyo itawanufaisha zaidi watanzania badala ya kampuni za kigeni hivyo kuwa na uchumi endelevu.
Mwandishi wa Makala haya ni Albano Midelo ambaye amesomea masuala ya mafuta,gesi,mafuta na mazingira mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa